Kampuni ya Selcom, inayojulikana kwa kutoa suluhisho za kifedha za kidijitali, imezindua mashine mpya ya Point of Sale (POS) katika maadhimisho ya Wiki ya Fedha yaliyofanyika Mbeya. Mashine hii inalenga kuboresha huduma za kifedha kwa wafanyabiashara na mawakala kwa kutoa suluhisho rahisi, salama, na lenye ufanisi zaidi kwa miamala ya kila siku, na hivyo kuongeza faida kwa biashara.
Vipengele vya Mashine Mpya ya POS ya Selcom Mashine hii mpya ya Selcom POS inakuja na teknolojia bora inayoongeza thamani kwa watumiaji wake kwa huduma mbalimbali zifuatazo:
1. Kutuma na Kupokea Pesa: Wakala au mfanyabiashara anaweza kutuma na kupokea pesa kutoka kwa mitandao yote ya simu na benki zote nchini kwa urahisi.
2. Kutoa Pesa: Mawakala wanaweza kutoa pesa kwa wateja kutoka kwenye mitandao yote ya simu na benki zote, kwa kutumia mashine hii mpya.
3. Floti Moja kwa Huduma Zote: Hii inamaanisha kuwa wafanyabiashara na mawakala wanaweza kutumia floti moja kufanya miamala ya kutuma na kupokea pesa kutoka kwa benki na mitandao yote ya simu. Hii inawaondolea usumbufu wa kuwa na floti kwa kila mtandao au benki tofauti.
4. Makato ya Chini kwa Miamala: Mashine hii mpya inaruhusu wafanyabiashara kufurahia viwango vya chini vya makato kwenye kila muamala, hivyo kusaidia kuongeza mapato.
5. Uhamisho wa Fedha: Huduma ya uhamisho wa fedha ni ya kasi na salama zaidi, ikihakikisha urahisi wa kufanya miamala ya haraka.
6. Malipo ya Kadi: Mashine hii inakubali malipo kutoka kwa kadi mbalimbali kama Visa, Mastercard, na American Express, pamoja na kutumia TanQR.
7. Malipo ya Bili: Watumiaji wa mashine hii wanaweza kulipia bili mbalimbali kama Luku, maji, bili za serikali, na nyinginezo.
8. Lipia Mizigo na Wafanyakazi: Inawawezesha wafanyabiashara kulipia mizigo ya biashara na mishahara ya wafanyakazi kwa urahisi.
9. Kubadilisha Namba ya Siri (PIN): Wafanyabiashara na mawakala wanaweza kubadilisha namba zao za siri kwa urahisi moja kwa moja kupitia mashine hii.
10. Taarifa za Akaunti: Wafanyabiashara wanaweza kupata taarifa za miamala yao papo hapo kupitia mashine hii.
11. Huduma kwa Wateja Masaa 24: Kitengo cha huduma kwa wateja cha Selcom sasa kinapatikana masaa 24 kupitia namba ya bure 0800 714 888, kuhakikisha msaada unapatikana muda wowote.
Mashine hii ya POS inapatikana kwa bei nafuu ya TZS 200,000 tu, ikiwa ni pamoja na floti ndani yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Selcom, Shumbana Walwa, alisema, “Selcom inajivunia kuzindua mashine hii mpya ya POS, inayowawezesha wafanyabiashara na mawakala kufanya miamala kwa urahisi, usalama, na kwa gharama nafuu. Tunaamini ubunifu huu utachangia ukuaji wa biashara ndogo ndogo na kusaidia upatikanaji wa huduma bora za kifedha nchini.”
Selcom ni kampuni inayoongoza katika utoaji wa huduma za kifedha za kidijitali nchini Tanzania. Kwa zaidi ya miaka ishirini ya kutoa huduma, kampuni hii imeendelea kutoa huduma za haraka, salama, na rahisi kwa wafanyabiashara na mawakala kote nchini.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea: www.selcom.net