Wakulima, wazalishaji wa mbegu na wasindikaji wa bidhaa za kilimo wameeleza kunufaika na ugunduzi wa mbegu zilizofanyiwa Utafiti na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika mazao ya karanga, maharage na mtama kwa kuwaongezea tija katika mnyororo mzima wa thamani wa mazao hayo.
Wameeleza hayo leo Oktoba 23, 2024 katika Mkutano uliofanyika Dodoma wa kutoa matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanyika zikilenga kubaini uhitaji wa soko na kusambaza mbegu mpya za mtama, maharage na Karanga.
Mkutano huo umeratibiwa na TARI kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Uboreshaji wa Mahindi na Ngano (CIMMYT).
Akieleza tija anayopata, Olipa Mahala- mzalishaji wa mbegu za karanga na mtama kutoka Wilaya ya Chamwino -Dodoma anasema awali alipokuwa akilima mbegu za kienyeji alikuwa anavuna gunia 4-5 kwa hekta lakini alipoanza kulima mbegu ya mtama ya TARISOR 1 anavuna wastani wa gunia 15-20 kwa hekta.
Kadala Komba- ni msindikaji wa siagi ya karanga kutoka Bahi anayetumia mbegu za karanga za Naliendele 2016 anasema imemuongezea tija kwa kupendwa sokoni kutokana na ladha pamoja na rangi yake.
Awali akifungua kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa TARI- Dkt. Thomas Bwana amesema TARI imegundua mbegu mbalimbali na inaendelea kufanya tafiti zaidi ili kugundua teknolojia zinazojibu changamoto za wakulima na wadau katika mnyororo mzima wa thamani.
Miongoni mwa mbegu ziligunduliwa na TARI ni aina mpya za mbegu za Maharage; TARIBEAN 6, TARIBEAN 7, TARIBEAN 8, TARIBEAN 9, TARIBEAN 10 na TARIBEAN 11.
Karanga aina za; TARIKA 1 na TARIKA 2 pamoja na mtama TARISOR 1 na TARISOR 2.
Dkt. Sophia Kashenge – Mkurugenzi wa Idara ya Uhaulishaji wa Teknolojia na Mahusiano wa TARI amesema TARI haishii kugundua bali pia kuhakikisha mbegu hizo zinawafikia wakulima kupitia njia mbalimbali ikiwemo uanzishaji wa mashamba darasa, kutoa elimu kwa maafisa ugani, wakulima, wazalishaji mbegu na wafanyabiashara wa mbegu na wasindikaji wa bidhaa.