Mwanachama wa Lutheran Church SACCOS, Bw. Onesmo Nyela Sanga, akipata maelezo kutoka kwa Bertha Hyera afisa wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) wakati alipotembelea katika banda hilo kwenye wiki ya huduma za Kifedha inayofanyika kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe jijini Mbeya katikati ni Thuwaiba Juma afisa kutoka DIB.
……………
Mwanachama wa Lutheran Church SACCOS, Bw. Onesmo Nyela Sanga, ameishukuru Bodi ya Bima ya Amana (DIB) kwa kumpa elimu na kumuelimisha kuhusu shughuli za bodi hiyo. Alieleza kuwa mara nyingi benki wanazofungua akaunti hazitoi taarifa kuhusu taasisi inayolinda amana zao, jambo linalosababisha wananchi kutoelewa umuhimu wa Bodi ya Bima ya Amana.
Onesmo ametoa shukrani hizo alipotembelea banda la DIB katika Wiki ya Huduma za Kifedha inayofanyika katika viwanja vya Luanda, Nzovwe, jijini Mbeya, leo Oktoba 23, 2024. Ameeleza kuwa amefaidika na elimu aliyoipata kutoka kwa maafisa wa bodi hiyo. “Nitakwenda kuwashauri wenzangu kwenye kikundi cha SACCOS na wengine ambao watahitaji elimu hii muhimu,” amesema Onesmo.
Pia ameuliza kama kuna gharama yoyote ya kujiunga na Bodi ya Bima ya Amana. Akijibu swali hilo, Afisa wa Bodi hiyo, Bi. Bertha Hyera, alisema, “Kwa mujibu wa sheria tunazozifanyia kazi kwa sasa, mwananchi wa kawaida hachangii. Anayechangia ni benki yako, hivyo kama unavyo akaunti kwenye Benki ya Biashara TCB, benki hiyo itachangia kwenye mfuko wa bima kwa niaba yako.”
Bi. Hyera ameongeza kuwa lengo la bodi hiyo ni kuhakikisha wananchi wanajua kwamba kuna taasisi inayowalinda endapo benki zao zitafungwa au kufilisika. “Kuna benki zimefungwa, na watu hawajui jinsi ya kuchukua pesa zao kwa sababu hawakuwa na uelewa kuwa walikuwa na haki kupitia taasisi ya serikali. Tunawaelimisha ili wawe mabalozi wetu, si tu kwenye SACCOS, bali pia kwa akaunti za watu binafsi,” amefafanua.
Bi. Hyera akijibu swali la mwananchi mmoja aliyeuliza nini cha kufanya baada ya kufungua akaunti. Alisema, “Ukishafungua akaunti na benki kukubali kuwa mteja wao, taarifa zako zinasomwa kwetu. Hivyo, tutajua ni benki gani unayoshirikiana nayo, na endapo itafungwa, moja kwa moja utarudishiwa pesa zako kupitia DIB.”
Bodi ya Bima ya Amana imeendelea kujibu maswali ya wananchi waliotembelea banda lao, ambapo Wananchi wengi wamefurahia elimu hiyo na kuahidi kuisambaza kwa wenzao katika makundi mbalimbali.
Mwanachama wa Lutheran Church SACCOS, Bw. Onesmo Nyela Sanga, akipata maelezo kutoka kwa Bertha Hyera afisa wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB) wakati alipotembelea katika banda hilo kwenye wiki ya huduma za Kifedha inayofanyika kwenye viwanja vya Luanda Nzovwe jijini Mbeya katikati ni Thuwaiba Juma afisa kutoka DIB.
Baadhi ya wanafunzi waliotembelea banda la DIB wakipata maelezo kutoka kwa Thuwaiba Juma Afisa wa Bodi ya Bima ya Amana.