………………,.
Na John Mapepele
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake ya Makumbusho ya Taifa, Chuo Cha Taifa Cha Utalii na Bodi ya Utalii kwa kazi nzuri ya maboresho makubwa yanayofanyika.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Timotheo Paul Mzava ambaye pia ni Mbunge wa Korogwe ameyasema haya leo Oktoba 23, 2024 wakati Kamati hiyo ilipokuwa ikipokea taarifa za utekelezaji wa taasisi hizo jijini Dodoma.
“Tunawapongeza Makumbusho ya Taifa kwa kazi nzuri inayofanya katika kipindi hiki kifupi na tunawataka muendelee kufanya maboresho makubwa ili maboresho haya yaweze kuleta mchango mkubwa kwenye mapato ya Taifa” amefafanua Mhe Mzava
Aidha, amewataka waongeze mikakati na ubunifu wa vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati wa miundombinu bila kuathiri uasili wake.
Pia amepongeza kwa ukarabati wa Makumbusho ya Azimio la Arusha iliyopo jijini Arusha ambayo amesema imekarabatiwa katika kipindi kifupi.
Ameitaka Wizara kukamilisha mara moja maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kwenye ziara yake ya hivi karibuni mkoani Ruvuma ya kutaka kujengwa kwa Makumbusho ya Marais ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii. Mhe, Balozi. Dkt. Pindi Chana alimhakikishia kuwa maelekezo hayo yalishaanza kutekelezwa mara moja na kuiomba Kamati hiyo kutembelea eneo la ujenzi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti naomba nimshukuru Mhe. Rais kwa maelekezo yake na tayari tumeshaanza utekelezaji wake mara moja na nitoe ombi kwa Kamati yako itembelee eneola ujenzi ambalo lipo hapa hapa Dodoma ili iweze kuendelea kutushauri na kutusimamia” ameongeza Mhe. Chana
Kwa upande wa Chuo Cha Taifa Cha Utalii, Mhe. Mzava amepongeza kwa mikakati iliyojiwekea na kutaka kiongeze mikakati ya kujitangaza.
Kuhusu Bodi ya Utalii ameitaka Wizara kuisaidia Bodi hiyo iweze kujitegemea ili itimize jukumu lake la kutangaza vivutio mbalimbali vya Utalii