Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM) Mhe. Mizengo Pinda, amekutana na kuzungumza na uongozi wa Jeshi la Polisi nchini Botswana alipotembelea Makao Makuu ya Jeshi hilo jijini Gaborone tarehe 21 Oktoba 2024..
Mhe. Pinda alikwenda katika ofisi hizo kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na ujumbe wake ambako alikutana na kuzungumza na Kamishna wa Polisi wa Botswana Bi. Dinah Marathe.
Mhe. Pinda na ujumbe wake walitembelea Ofisi za Jeshi la Polisi kwa lengo la kujitambulisha kama Mkuu wa Misheni ya uangalizi ya SADC na ujumbe wa misheni hiyo ambao wako nchini Botswana kwa ajili ya kazi ya Uangalizi wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Mhe.Pinda aliambatana na Sekretarieti ya SADC, wajumbe wa SADC Organ TROIKA, Baraza la Ushauri wa Uchaguzi la SADC, na Waangalizi wa SADC.
Mhe. Pinda aliwaambia maafisa hao wa Polisi kuwa SEOM ipo nchini Botswana kwa ajili ya kutekeleza jukumu la uangalizi katika uchaguzi huo ambalo wamekabidhiwa na SADC ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuimarisha demokrasia katika nchi za ukanda huo.
Mhe. Pinda alielezea jinsi SEOM ilivyojipanga kutekeleza jukumu hilo ambapo wametoa mafunzo kwa waangalizi wao ili wajue taratibu na miongozo ya kufuata wakati wa kutekeleza jukumu hilo.
ziara hiyo ya Mhe. Pinda pia ililenga kufahamu jinsi Jeshi la Polisi nchini humo lilivyojipanga kuelekea kwenye uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
Akizungumza katika kikao hicho Kamishna wa Polisi wa Botswana Bi. Marathe alimkaribisha Mkuu wa Misheni ya SEOM na ujumbe wake nchini Botswana na kumshukuru kwa kwenda kuwatembelea na kuahidi kushirikiana nao katika kutekeleza jukumu hilo muhimu kwa Jumuiya na nchi yao kwa ujumla.
Amesema Jeshi la Polisi la Botswana limejipanga kikamilifu kuhakikisha Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo unafanyika kwa amani na utulivu na nchi kuendelea kuwa na usalama.
Alisema Botswana ni nchi ya amani na kwamba askari wa nchi hiyo hutembea bila silaha na kuongeza kuwa maafisa wa polisi nchini humo wako tayari kutekeleza kikamilifu majukumu yao katika kipindi chote cha uchaguzi kwa kuendelea kulinda amani, raia na mali zao.