Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amevitaka Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo (SACCOS) kutumia mifumo ya kidigitali inayoendana na uwezo wa kifedha wa vyama hivyo, ikiwemo mfumo unaosimamiwa na Muungano wa SACCOS nchini (SCCULT).
Akizungumza katika uzinduzi wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Duniani leo tarehe 21 Oktoba 2024, jijini Mwanza, Mhe. Silinde alieleza kuwa mfumo huu umeundwa kwa kuzingatia mazingira na mahitaji ya SACCOS nchini. Alisisitiza kuwa SCCULT itaendelea kusimamia utekelezaji wa mfumo huo ili kuhakikisha vyama vinapata usimamizi mzuri.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Ulimwengu Mmoja Kupitia Ushirika wa Kifedha”. Mhe. Silinde aliongeza kuwa matumizi ya TEHAMA ni muhimu kwa SACCOS endapo zinataka kuwahudumia wanachama wao kwa ufanisi na kukabiliana na ushindani uliopo kwenye soko la fedha. Aliwahimiza kutumia mfumo wa MUVU katika kuendesha na kusimamia shughuli za vyama, akibainisha kuwa ni wakati sasa kuacha mazoea ya kutumia makaratasi na kujiendesha kiholela.
“Nafahamu kumekuwa na mazoea ya kupuuza maelekezo na ushauri unaotolewa ili kuboresha sekta, lakini sasa ni muhimu kwa SACCOS kufuata miongozo ili kuboresha utendaji wao,” alisema Mhe. Silinde.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya SCCULT, Khajat Aziza Mshana, alisema kuwa maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya 76 duniani tangu kuanzishwa kwake na mara ya 15 hapa nchini. Alibainisha kuwa SACCOS zina ushawishi mkubwa katika kuunganisha jamii kwa kutoa huduma zinazobadilisha maisha ya wanachama na jamii kwa ujumla.
Naye Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege, alieleza kuwa Tume imepokea maombi 1,211 ya leseni kutoka kwa SACCOS, na hadi sasa imetoa leseni 963 kwa SACCOS zilizokidhi vigezo kwa mujibu wa sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha.
“Viongozi wa SACCOS wanapaswa kuendelea kutekeleza matakwa ya sheria, kanuni na miongozo kwa kufanya mikutano mikuu ya mwaka, kuwasilisha bajeti mapema, na kufungua matawi na milango ya huduma kwa mujibu wa sheria. Kuendesha matawi bila idhini ya Mrajis ni kosa la jinai,” alisema Dkt. Ndiege.