…………………
Na Sixmund Begashe – Busega, Simiyu.
Serikali ya Wilaya ya Busega imeihakikishia Wizara ya Maliasili na Utalii kuendeleza ushirikiano uliopo katika kulinda maliasili, kuendeleza utalii pamoja na kuwalinda wananchi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu ili kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa Wilayani Busega, Mkoa wa Simiyu, na Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mheshimiwa Faidha Suleiman Salim, kwenye kikao kazi kati ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, maafisa wa wizara, na Kamati ya Usalama ya Wilaya hiyo.
Mhe. Salim ameeleza kuwa, ingawa Wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu, inapata ushirikiano mzuri kutoka kwa Jeshi la Uhifadhi pale wanapohitajika kwa haraka, hasa wakati kunapotokea wanyamapori kama vile viboko, mamba, na fisi.
Aidha, Mhe. Salim amemhakikishia CP Wakulyamba kuwa Serikali ya Wilaya hiyo itafanyia kazi ushauri alioutoa, hususan kuhusu ushirikiano katika ulinzi wa mipaka ya maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kulima mazao ambayo si rafiki kwa wanyamapori, na kuunda vikundi vya vijana kupambana na wanyamapori hao, huku akiishauri wizara hiyo kutoa kipaumbele cha vitendeakazi kwa vikundi vya vijana vitakavyo undwa.
Akizungumzia ziara hiyo, CP Wakulyamba amesema nia ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuona wananchi wanaishi kwa amani bila kubughudhiwa na wanyamapori wakali na waharibifu, sambamba na kuhakikisha maeneo yaliyohifadhiwa kisheria kulindwa ili kuwanufaisha wananchi wote wa sasa na vizazi vijavyo.
“Ni vyema jamii iunge mkono juhudi za serikali katika kufikia malengo yaliyopo kwa uhifadhi endelevu na utalii” amesema CP. Wakulyamba.
CP Wakulyamba ameeleza kwamba lengo la ziara hiyo ni kufuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyotoa akiwa kwenye ziara Mkoani Simiyu sambamba na kukagua utendaji kazi wa Taasisi zinazounda Jeshi la Uhifadhi zilizoko Mikoa ya Kanda ya Ziwa Victoria.
Katika ziara hiyo, Kamishana Wakulyamba ametembelea mapori ya akiba ya Maswa, Kijereshi na kukagua eneo la Nyantwali (Speakgulf) ambalo wananchi wanaendelea kulipwa fidia ili libaki kwa matumizi ya wanyamapori.