Na Elimu ya Afya kwa Umma.
Kufuatia Serikali kupitia Wizara ya Afya kuendelea na jitihada mbalimbali za uelimishaji kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ya Afya kwa njia ya Matangazo ya Redio na Televisheni, Wananchi Mkoani Njombe wamefurahia hatua hiyo kwani imebadilisha tabia na kuwa na mwitikio wa kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za afya katika kuboresha afya ya Mama na Mtoto.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya Wananchi hao wamesema matangazo ya elimu ya Afya yanayochezwa kupitia redio yamesaidia akina baba kubadili tabia na kuwa na mwitikio kwa wanaume kuambatana na wenza wao katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
“Matangazo kuhusu afya tunayasikia , lakini mwanzoni hamasa ilikuwa ya chini akina baba kwenda kituo cha kutolea huduma ya afya mfano mimi mwenyewe nilikuwa sipendi kwenda na mama kliniki na baada ya matangazo haya ya elimu ya afya yanayochezwa redioni na kwenye TV ninashukuru sana ninaambatana na mke wangu kliniki bila wasiwasi wowote”amesema mmoja wa wananchi.
Halikadhalika, wameelezea kuhusu tangazo la Ugonjwa wa Nimonia lilivyowaingia moyoni mwao na kubainisha kuwa limesaidia umuhimu wa kutambua dalili za mapema na kuwahi kituo cha kutolea huduma za afya.
Ikumbukwe kuwa Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wadau ikiwemo Shirika linalijihusisha na uandaaji wa Matangazo yenye jumbe mbalimbali kuhusu Elimu ya Afya “Development Media International Associates (DMI) imekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa Elimu ya afya kupitia vyombo vya Habari ikiwemo redio, televisheni na mitandao ya Kijamii lengo likiwa ni kubadili tabi katika jamii na kuweza kuokoa maisha.