Na Ashrack Miraj (Fullshangwe Media)
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, ameanza kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mkazi kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa/Kitongoji unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza katika ziara yake, DC Kasilda amewahimiza wananchi ambao bado hawajajiandikisha kutumia siku mbili zilizobaki kufika kwenye vituo vya kujiandikisha. Ameeleza kuwa uchaguzi huu ni muhimu kwa ustawi wa taifa kwani utatoa mwelekeo wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 unaohusisha nafasi za Rais, Wabunge, na Madiwani.
Amefafanua kuwa Wilaya ya Same ina jumla ya vitongoji 503, ambapo kila kitongoji kinatambulika kama kituo cha kujiandikisha. Zozi la uandikishaji linafanyika kwa siku kumi, kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024, na wananchi wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili kuweza kushiriki katika uchaguzi wa viongozi wa maeneo yao.
Aidha, DC Kasilda amesisitiza kuwa kitambulisho cha mpiga kura kinachotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2025. Hata hivyo, kwa uchaguzi wa Mtaa/Kitongoji mwaka huu, ni lazima wananchi wawe wamejiandikisha kwenye daftari la mkazi ili waweze kupiga kura.