***************
Na Sixmund Begashe – Simiyu
Jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii za kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu zimepongezwa na Viongozi wa Wilaya za Meatu, Itilima na Bariadi na kuwa jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na wananchi wote ili kuondokana na changamoto hiyo.
Hayo yamejili kwenye vikao kazi vilivyofanywa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba na uongozi wa Wilaya hizo na Vijiji kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja wa namna ya kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu hasa Tembo pamoja na uhifadhi endelevu wa Maliasili.
Katika kikao kazi hicho, Mkuu wa Wilaya ya Meatu Mhe. Faudhia Ngatumbura amesema, ziara hiyo ya CP. Wakulyamba na viongozi wengine wa Wizara imeleta faraja kubwa kwa wananchi wa Wilayani hiyo na kuwa Ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano wakutosha kwa Wizara katika kuhakikisha wananchi wanaishi bila kubugudhiwa na wanyamabori hao.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wengine wa vijiji vya Mwagwila na Mwanyahina, Diwani wa Kata ya Mwanyahina, Mhe. Nawida Jibunge Mawida amesema ziara hiyo itasaidia kuimarisha vikundi vya Kijamii walivyo unda vya kupambana na Wanyamapori wakali na waharibifu kwa kuwa Wizara imeahidi kuwapatia mafunzo vijana kwenye vikundi hivyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bariadi Mhe. Saimon Simalenga licha ya kuainisha madhara yanayotokana na Wanyamapori wakali na waharibifu, amesema Ofisini yake itaendelea kushirikiana na Wizara katika kupambana na Ujangili ili kuimarisha Uhifadhi na kuvutia watalii Wilayani humo hali itakayopelekea kuinua uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kifutajasho na Kifutamachozi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Bi. Mwanana Mssumi emesema kwa mwaka 2020,2021 na 2022 Serikali imeipatia Wilaya hiyo zaidi Milioni 300 kama Kifutamachozi na Kifutajasho, jambo linaloleta faraja kubwa kwa wananchi walioathiriwa na Wanyamapori wakali na waharibifu.
Akiendesha vikao hivyo CP. Wakulyamba amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya jiditihada kubwa za kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu hususani Tembo, ni pamoja na kununu vifaa vya kisasa, kuongeza ajira za askari wa Uhifadhi, kuimarisha uwezo wa Jeshi la Uhifadhi, hivyo ni vyema jitihada hizo zikaungwa mkono na wananchi wote ili kwa pamoja kufikia lengo la kumaliza changamoto hiyo.
Akiwa ameambatana na Kamishna Msaidi wa Uhifadhi TAWA, Saidi Kabanda, Viongozi waandamizi kutoka TAWA, Wizara ya Maliasili na Utalii na Jeshi la Polisi, CP. Wakulyamba amewashauri viongozi wa Wilaya hizo kuhakikisha wanaanzisha vikundi vya Vijana vya kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu na kuwa Wizara itasaidia kutoa mafunzo stahiki ili kuwajengea uwezo vijana hao.