Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akimtambulisha Mkandarasi kutoka Kampuni yaShandong Luqiao Group kwa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi huyo eneo la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka
(km 50) kwa kiwango cha lami, Mkoani Kagera leo tarehe 18 Oktoba, 2024.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiteta jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi kampuni ya Shandong Luqiao Group eneo la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami,
Mkoani Kagera leo tarehe 18 Oktoba, 2024.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wakati wa wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Kampuni ya Shandong Luqiao Group eneo la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami, Mkoani
Kagera leo tarehe 18 Oktoba, 2024.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Eng. Dkt. Christina Kayoza akitoa taarifa wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Kampuni ya Shandong Luqiao Group eneo la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami, Mkoani Kagera leo tarehe 18 Oktoba, 2024.
Wananchi wa Wilaya ya Kyerwa wakimsiliza Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa wakati wa hafla ya kumkabidhi Mkandarasi Kampuni ya Shandong Luqiao Group eneo la mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami, Mkoani Kagera leo
tarehe 18 Oktoba, 2024.
Muonekano wa sehemu ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami ambayo inagharamiwa kwa Shilingi Bilioni 94.34. Ujenzi wa barabara hiyo inaunganisha Wilaya ya Kyerwa na Karagwe Mkoani Kagera.
…………..
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemtambulisha kwa Wananchi na kumkabidhi eneo la mradi Mkandarasi Kampuni ya Shandong Luqiao Group atakayeanza ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka (km 50) kwa kiwango cha lami na kuuagiza Wakala ya Barabara
(TANROADS) kumsimamia Mkandarasi huyo ili barabara hiyo ikamilike kwa wakati bila ya kusuasua.
Hafla ya kumkabidhi Mkandarasi imefanyika leo Oktoba 18, 2024 katika eneo la Rwenkorongo Wilayani Kyerwa ambapo Bashungwa ameeleza ujenzi wa barabara utaziunganisha Wilaya za Karagwe na Kyerwa kwa kugharamiwa na Serikali kwa Shilingi Bilioni 94.34.
“Mheshimiwa Rais anatambua wanaKyerwa walikuwa na kiu kubwa na barabara hii ndio maana ametoa kibali ili niweze kufika hapa na kumkabidhi Mkandarasi huyu kwenu ili aweze kuaza ujenzi na kuwaondolea wananchi kero ya usafiri mliyokuwa mnaipata”, amesisitiza Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Mkandarasi kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo iliyokuwa inaishia Kata Chonyonyo na kuunganisha kipande cha kilometa 11 hadi kufika Omurushaka ambapo TANROADS wanaendelea na taratibu za kimkataba.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka utafungua fursa mpya za Kibiashara, Uchumi na Uwekezaji pamoja na kuchochea shughuli za utalii katika Mbuga za Taifa za Ibanda, Burigi Chato, Rubondo na Rumanyika zilizopo katika Mkoa wa Kagera na Geita.
Aidha, Bashungwa amebainisha mikakati ya Serikali ya kuendelea kuifungua Wilaya ya Kyerwa kwa barabara za lami ambapo ameeleza barabara Omurushaka – Kyerwa itakuwa na mwendeleo hadi Murongo (Km 112.11) na kuunganisha Mji wa Nkwenda na Nyakaiga pamoja na
kupendezesha mji wa Kaisho na Nkwenda kwa barabara za lami.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Mkoa huo ikiwemo Sekta ya Afya, Maji, Umeme, Elimu,
Kilimo na Miundombinu ya barabara.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara (TANROADS), Eng. Dkt. Christina Kayoza ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Kyerwa – Omurushaka utatekelezwa kwa muda wa miezi 36 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2027 ambapo hadi sasa Serikali
imeshalipa malipo ya awali ya Shilingi Bilioni 9.3 kwa Mkandarasi ili aendelee na maandalizi ya kuanza kazi.