Na Neema Mtuka
Serikali, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imeanza usambazaji wa umeme katika vitongoji 75 vya Mkoa wa Rukwa, baada ya kukamilisha kusambaza nishati hiyo kwenye vijiji 320 kati ya 339 vilivyopo mkoani humo.
Mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 15.7 unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 24 na unalenga kunufaisha zaidi ya kaya 33,000.
Akizungumza leo, Oktoba 16, 2024, wakati wa hafla fupi ya kumtambulisha mkandarasi, STEG International Services kutoka Tunisia, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Daudi Ssebiga, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa Makongoro Nyerere, amesema kuwa kufikishwa kwa umeme katika vitongoji hivyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza umasikini miongoni mwa wananchi.
Mhandisi Ssebiga aliongeza kuwa umeme vijijini utasaidia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, pamoja na kuboresha maisha ya wananchi kwa ujumla. “Umeme ni nguzo muhimu katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuleta tija kwa wananchi. Nishati hii, ikitumiwa ipasavyo, itawainua kiuchumi na kupunguza ugumu wa maisha,” alifafanua.
Awali, Msimamizi wa Miradi ya REA katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Danstan Kalugira, alitoa taarifa ya mradi huo, akisema kuwa kati ya vijiji 339 vya Rukwa, vijiji 320 tayari vimepatiwa umeme. Vijiji vilivyosalia 19 viko katika hatua za mwisho za ukamilishaji na vitapata umeme karibuni.
“Kwa kipindi cha miaka miwili ijayo, vitongoji 75 katika majimbo matano ya Mkoa wa Rukwa vitapatiwa umeme kupitia mradi huu, ambao utekelezaji wake umeanza,” alieleza Mhandisi Kalugira.
Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Sumbawanga Mjini, Nkasi Kusini, Nkasi Kaskazini, Kwela, na Kalambo.
Mhandisi Kalugira alimhakikishia Kaimu Katibu Tawala kuwa REA imejipanga kuhakikisha umeme unafika kwenye vitongoji vyote, huku utekelezaji ukiendelea kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya STEG International Services, Aymen Louhaichi, ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu, akibainisha kuwa maandalizi yote muhimu tayari yameanza.
Wananchi wa kijiji cha Ntatumbila, wilayani Nkasi, akiwemo Siwema Dickson, wameelezea furaha yao kuhusu mradi huo, wakisema kuwa upatikanaji wa umeme utawasaidia kuondokana na umasikini na kujipatia fursa za kujikwamua kiuchumi.