Na Sophia Kingimali.
TAASISI ya Uhasibu Tanzania (TIA), imesaini mkataba na kampuni ya Salem Construction kwaajili ujenzi wa jengo la kampasi yake mkoani Singida huku wakimtaka mkandarasi kuhakikisha anafanyakazi kwa karibu na wazawa wa maeneo hayo kwa kutoa ajira ambapo ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 13.5.
Akizungumza leo Oktoba 15,2024 katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye ofisi za taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TIA, Prof. William Pallangyo amesema fedha za ujenzi wa kampasi hiyo zimetolewa chini ya Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi kwa Vyuo Vikuu nchini (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Aidha amemtaka mkandarasi kuhakikisha anajenga jengo lenye ubora na kufanyakazi kwa karibu na wananchi wa Singida ili wawe walinzi wa mradi huo mpaka utakapokamilika kwa muda ambao umewekwa.
“Tumemtaka mkandarasi azingatie kanuni za ujenzi ili kuhakikisha wafanyakazi wanakuwa salama wakati wote tunataka mpaka mradi unapokamilika watu wawe salama kusitokee kifo hata kimoja wala majeruhi,” amesema Prof. Pallangyo.
Aidha ameongeza kuqa Mkataba huo utachukua miezi 24 hadi kukamilika kwa ujenzi jengo hilo na amemtaka mkandarasi kuhakikisha anakamilisha kwa wakati.
Amesema wataendelea kufanyakazi kwa karibu na benki ya dunia ambayo ndiyo inayofadhili mradi huo ili kuhakikisha kila mkandarasi anapoomba malipo analipwa kwa wakati ili mradi usisimame.
Kwa upande wake Mratibu wa HEET Kitaifa, Dkt. Kenedy Hossea, ameipongeza TIA na menejimenti yake kwa kupata mkandarasi mapema kwaajili ya ujenzi wa jengo katika Kampasi ya Singida
“Nawapongeza Mtendaji Mkuu wa TIA kwasababu kuna watu walianza muda mrefu hawajapata mkandarasi mpaka sasa wanalumbana tu zabuni inatangazwa inafutwa wanashindwa kufikia muafaka,” amesema
Pamoja na hayo, Dkt. Hossea amemtaka mkandarasi wa jengo hilo kuzingatia ubora na kuahidi kuwa wataalamu wanaosimamia mradi huo kutoka wizarani watakuwa wakipita mara kwa mara kuhakikisha ubora unazingatiwa.
Nae Mwakilishi wa Salem Construction, Charles Casmir, amesema mkataba huo ni wa miezi 24 lakini wao wamejipanga kukamilisha mradi huo ndani ya miezi 18.
Amesema wanatarajia kuwa jengo hilo litakuwa la mfano lakini pia watahakikisha wanazingatia usalama wa wafanyakazi na jamii inayozunguka mradi huo katika Mkoa wa Singida.