Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Kampuni ya Mafia Promotion Boxing imetoa msaada wa majiko ya gesi kwa wanawake wanaouza vyakula katika masoko ya Mgandini, Makorora, na Mlango wa Chuma, jijini Tanga. Pia imetoa misaada kwa kituo cha kulea watoto yatima cha Green Instead Orphanage Foundation kilichopo Bombo, ikiwa ni sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii.
Ikumbukwe kuwa mabondia wanaodhaminiwa na kampuni hiyo walishinda mapambano yao yaliyofanyika Oktoba 5, 2024, jijini Dar es Salaam. Ushindi huo, uliochagizwa na pambano maarufu lililojulikana kama “KO ya Mama,” ulileta heshima kwa taifa, huku Rais Samia Hassan akiwatunuku zawadi mabondia hao, jambo lililowapa motisha zaidi katika kuendeleza mchezo wa ngumi nchini.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi wa Matangazo na Uzalishaji wa Mafia Promotion, Omari Clayton, alisema kuwa mbali na kurudisha fadhila kwa jamii, kampuni hiyo inaunga mkono kampeni ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kuachana na mkaa na kuni. Hii ni kwa lengo la kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa na mabadiliko ya tabianchi.
“Kampuni ya Mafia Promotion Boxing inaunga mkono juhudi za Rais wetu mpendwa katika kupambana na matumizi ya mkaa. Ndiyo maana tumeamua kutoa majiko ya gesi kwa wanawake wanaofanya biashara ya kupika katika masoko ya jiji la Tanga,” alisema Clayton.
Akiongea kwa niaba ya mabondia wenzake, Ibrahim Mafia alisema ushindi wao haukuwa rahisi, lakini walipata nguvu kutokana na maombi ya Watanzania. “Ule ushindi ni wetu wote, Watanzania. Tumepokea zawadi kutoka kwa Rais wetu, tukaona tushirikiane kile tulichopata kwa kuwasaidia wenzetu.”
Ibrahim Mafia alimshinda mpinzani wake, Enoch Tettey kutoka Ghana, katika pambano la kuwania mkanda wa dunia wa ‘World Boxing Council Bantamweight’ kwa uzito wa kilogramu 53, kwenye ukumbi wa City Center Hall, Magomeni Sokoni, na kumshinda kwa KO.
Baadhi ya wanawake waliopokea msaada wa majiko ya gesi wameishukuru Mafia Promotion Boxing kwa msaada huo. Walisema msaada huo utawasaidia kupunguza changamoto za matumizi ya mkaa na kurahisisha kazi zao za kupika.
“Tunawashukuru sana kwa msaada wenu, na Mungu atawalipa. Tumekuwa na changamoto ya mkaa, lakini sasa kupitia majiko haya, itarahisisha shughuli zetu za kila siku. Pia tunamshukuru Rais Samia kwa jitihada zake,” walisema.