Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media, Tanga
Wakati zoezi la uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Mkazi likiingia siku ya sita, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mkoani Tanga, Japhari Kubecha, ameibukia katika Stendi ya zamani ya mabasi Barabara 12, Jijini Tanga, na maeneo mbalimbali ya wananchi, kuwahamasisha kushiriki katika zoezi hilo muhimu. Lengo ni kuhakikisha wanajiandikisha ili waweze kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza na wananchi waliokusanyika stendi na kwenye vijiwe, DC Kubecha aliwasihi kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao baada ya kujiandikisha. Alisisitiza kuwa kuchagua viongozi bora ni njia ya kupata maendeleo na suluhisho la changamoto zinazowakabili.
“Kupiga kura ni haki yenu, wananchi wa Tanga. Hakikisheni mnachagua viongozi watakaoweza kubeba na kutatua matatizo yenu kwa miaka mitano ijayo. Maendeleo ya Wilaya ya Lushoto yataletwa na sisi wenyewe, wana Tanga,” alisema DC Kubecha.
Zoezi la uandikishaji wananchi kwenye Daftari la Mkazi lilianza Oktoba 11, 2024, na litaendelea hadi Oktoba 20, 2024. Wananchi wanahimizwa kujiandikisha kwa wingi ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa demokrasia ya nchi.