Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) tarehe 12 Octoba 2024, ameungana na wananchi wa Wilayani Magu mkoani Mwanza kwenye mapokezi ya Mwenge wa Uhuru na kushuhudia baadhi ya miradi ya maendeleo ikizinduliwa na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Bw. Geofrey Eliachim Mzava.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa miradi wa maji wa Kihangara na mradi wa Kituo cha Afya cha Nyanguge kwa nyakati tofauti Mhe Dkt. Stegomena amempongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayofanya bila kuchoka ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia miradi mbalimbali.
Waziri Stergomena Tax amesema kuwa, Kahangara kilio kikubwa na changamoto kubwa ilikuwa ni maji safi na salama kwa muda mrefu kwa mapenzi makubwa ya Rais amehakikisha maji sasa yanapatikana na hivyo changamoto hii imekwisha.
Aidha, Waziri Stergomena pia akatoa wito kwa wananchi wa Magu kwa kuwataka kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2024 mpaka tarehe 20 Oktoba,2024 kushiriki zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura hivyo akawasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili waweze kuchagua viongozi watakaowaletea maendeleo kama hayo, Kwa sababu viongozi bora watakaofanya kazi na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ndiyo wale watakaowaletea maendeleo.
Awali akimkaribisha Waziri wa Ulinzi na JKT aongee na wananchi, Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Joshua Nasari alimpongeza Dkt. Stergomena Tax kwa kusema kuwa huyu ni mwana Magu na mwana Kahangara kuwa anavyo vinasaba vya Kahangara hivyo akamkaribisha kuongea kuhusu mradi huu.
Kwa upande wake Kiongozi wa Mbio za Mwenge mwaka 2024 Bw. Geofrey Eliachim Mzava, amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Magu Mhe. Joshua Nasari kwa kusimamia vyema mradi huu wa maji kwa kufuata taratibu za manunuzi na pia kutangaza zabuni na kuzingatia matumizi bora ya fedha za Serikali.
Mwenge wa Uhuru unaendelea za ziara Wilayani Magu ambapo miradi mbalimbali ya Maendeleo inaendelea kuzinduliwa na utafikia kilele tarehe 14 Oktoba, 2024 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan.