Na Sophia Kingimali.
Wajasiliamali wadogo wadogo nchini wameaswa kuchangamkia fursa za maonesho ya bidhaa zao pindi zinapojitokeza ili kuweza kujitangaza na kujifunza ili waweze kuziendeleza na kuboresha bidhaa zao.
Wito huo umetolewa na mwanzilishi wa Soko Swahili Market Catherine John(kate John) wakati akizungumza na mwandishi wa Fullshangwe kuhusu tamasha kubwa linalowakutanisha wajasiliamali wadogo linalotarajiwa kufanyika octoba 26,2024 katika viwanja vya Farasi Ostabay Jijini Dar es salaam.
Amesema lengo la Tamasha hilo ni kuwakutanisha wajasiliamali ili waweze kubadilishana uzoefu lakini pia kujifunza kwa wengine na namna ya kufanya biashara zao kuwa bora zaidi.
“Tamasha la Soko Swahili Market linawakutanisha wajasiliamali wadogo ambao wanazalisha bidhaa mbalimbali kama mafuta,watengenezaji wa sabuni,vitu vya asili,wabunifu wa mavazi,wauzaji wa matunda,mboga mboga na bidhaa nyingi ambazo sinazalishwa hapa nchini”,Amesema Catherine.
Ameongeza kuwa katika Tamasha hilo wanatarajia watu mbalimbali kwenda kuangalia bidhaa za Watanzania hivyo ni fursa kwa wazalishaji wadogo kujitokeza kwa wingi ili kutangaza bidhaa zao.
“Niwaombe watanzania na wasiowatanzania wajitokeze kwa wingi ili kuwatia moyo wajasiliamali wetu hapa nchini lakini pia kujivunia vya kwetu na kujionea wabunifu na wauzaji wa bidhaa zetu ambazo zinazalishwa nchini kwetu na zinachangia kodi yetu”,Amesema.
Aidha Catherine amesema kuwa mpaka sasa wajasiliamali zaidi ya 30 wameshajiandikisha kushiriki na zoezi hilo la kujiandikisha linatarajiwa kufungwa octoba 18 ambapo kiwango cha kushiriki ni sh elfu 70 kwa kila mjasiliamali.
Tamasha la Soko Swahili Market kwa sasa linafanyika kwa mara ya tatu tangu kuanzishwa kwakwe na lengo likiwa kuhakikisha kila mkoa Tanzania unashiriki.