Na Ashrack Miraji, Full Shangwe Media, Tanga
Zoezi la uandikishaji wa wananchi kwenye Daftari la Mkazi limeanza rasmi Oktoba 11 hadi 20 katika Wilaya ya Tanga, Mkoani Tanga. Ili kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika zoezi hili muhimu, kulifanyika mazoezi ya pamoja (Jogging) yaliyoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Hashim Kubecha. Lengo kuu la mazoezi hayo lilikuwa kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha, hatua muhimu itakayowawezesha kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, DC Kubecha alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandikisha kwenye Daftari la Makazi. Aliwataka wananchi kuwahimiza majirani, marafiki na familia zao kuhakikisha wanatumia vizuri siku hizo kumi za uandikishaji ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa kuchagua viongozi wa Serikali za Mitaa ambao watawaongoza kwa miaka mitano ijayo.
“Uchaguzi huu ni muhimu sana ndugu zanguni, na ndiyo maana leo tumeamua kufanya mazoezi haya ili kusisitiza umuhimu wa Uchaguzi wa mwaka huu. Uchaguzi wa mwaka huu unatoa dira ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 wa kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani,” alisema DC Kubecha.
Mazoezi hayo yalihudhuriwa na vikundi mbalimbali vya mazoezi ikiwemo Mkwakwani Fitness, Tanga Kwanza, Tanga Social Runners, Tanga Raha, Bomboka, Macechu Jogging, Galanos, Coastal Union, FFU, na wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Tanga.