*Ataka wawe mstari wa mbele, wasimame kwa hoja na kujipanga kimkakati kufanikisha ushindi wa CCM
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka vijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuzingatia ushindani wa hoja na kujipanga kimkakati, ikiwa ni maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.
Balozi Nchimbi, akizungumza kwenye hitimisho la matembezi ya vijana ya kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere, aliweka wazi kuwa ushindi wa CCM katika uchaguzi huo utategemea jitihada za vijana hao, akisisitiza kuwa vijana wa UVCCM wanapaswa kuwa tayari kupambana usiku na mchana kuhakikisha chama kinapata ushindi mkubwa wa kihistoria.
Aliwahimiza vijana hao kutochukulia ushindi wa CCM kwa urahisi, bali kuelewa kuwa ni matokeo ya juhudi na mikakati thabiti. “Mnapaswa kushindana kwa hoja, mkifanya kazi kwa bidii kuhakikisha CCM inashinda kwa namna ambayo wapinzani hawajawahi kushindwa,” alisema Balozi Nchimbi.
Akizungumzia umuhimu wa matembezi ya vijana yaliyofanyika kutoka Butiama hadi Nyamagana, alitoa pongezi kwa UVCCM kwa juhudi zao na akasema kuwa matembezi hayo yameleta faraja kubwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa vijana ni nguzo muhimu kwa ustawi wa CCM na Taifa, na kwamba wao ndio wana jukumu kubwa la kuendeleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia. Alimalizia kwa kuwahimiza vijana kushikamana na wazee wa chama ili kufanikisha ushindi wa kihistoria katika uchaguzi ujao.