Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limekuja na mikakati mipya inayolenga kusaidia Watanzania wenye kipato cha chini kumiliki nyumba bora kupitia bunifu za malipo nafuu. Moja ya mikakati hiyo ni mpango wa “mpangaji mnunuzi,” unaomuwezesha mpangaji kumiliki nyumba kupitia malipo ya awamu kwa muda mrefu.
Akizungumza katika Maonesho ya Saba ya Teknolojia ya Madini mkoani Geita, Afisa Mauzo na Masoko wa NHC, Ahmad Mwangu, amesema kuwa shirika hilo linatoa nyumba kwa gharama nafuu, ikiwemo nyumba za vyumba viwili kwa milioni 49 na vyumba vitatu kwa milioni 72. Mipango ya malipo inagawanyika katika miaka 5, 10, na 15, ambapo mpangaji anaweza kuanza kwa kulipa asilimia 10 ya malipo ya awali na kisha kumalizia kiasi kilichobaki kwa kulipia kidogo kidogo kila mwezi.
Mwangu amesema kuwa mpango huo ni nafuu kwa mtu wa kipato cha chini, kwa mfano mtu anayepata kipato cha shilingi 15,000 kwa siku anaweza kutumia kiasi hicho kwa siku 30, ambacho ni sawa na shilingi 450,000 kwa mwezi, kumudu malipo ya nyumba kwa kipindi cha miaka 15.
“NHC imeweka mikakati ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kumiliki nyumba bora bila kulazimika kulipa kiasi kikubwa mara moja,” amesema Mwangu. Pia amewataka wananchi kufika kwenye banda lao ili kupata maelezo zaidi kuhusu miradi hiyo na fursa za kumiliki nyumba.
NHC pia inatekeleza miradi mingine mikubwa ya ujenzi wa nyumba katika mikoa mbalimbali kama Dar es Salaam, Dodoma, na Arusha, ikiwemo viwanja vya bei nafuu kwa ajili ya ujenzi.