Bodi ya Bima ya Amana imeeleza kuwa jukumu lake kuu ni kuhakikisha wateja wa benki wanarudishiwa fedha zao pale benki inapopata changamoto au kufilisika, ili kuzuia hasara ya asilimia 100 kwa wananchi waliohifadhi fedha zao.
Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Isack Kihwili, alibainisha hayo leo, Oktoba 12, 2024, katika Maonesho ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya EPZ, Bombambili, Geita. Kihwili alisema bodi hiyo inatoa elimu kwa wananchi ili kuwafahamisha namna wanavyoweza kunufaika na ulinzi wa amana zao kupitia bodi hiyo.
“Sisi ni taasisi ya serikali yenye jukumu la kukinga amana za wateja, ambapo amana ni fedha ambazo watu wanahifadhi katika benki,” alisema Kihwili.
Alifafanua kuwa ingawa Bodi ya Bima ya Amana haiwezi kulipa fidia ya asilimia 100, kiwango cha fidia kimewekwa kuwa shilingi milioni 7.5 kuanzia Februari 2023. Kiasi hiki kitatolewa kwa wateja wa benki ambayo imepata changamoto ya kufilisika.
“Utaratibu ni kwamba hatulipi asilimia 100 ya fidia, lakini kiwango kilichowekwa ni milioni 7 na laki 5. Iwapo mteja alikuwa na kiasi chochote kinachozidi kiwango hicho, atarudishiwa fedha zake hadi kufikia milioni 7.5 bila kujali hali ya benki husika,” aliongeza Kihwili.
Alieleza kuwa endapo mteja alikuwa na kiasi cha chini ya milioni 7.5, atalipwa fedha zote kwa utaratibu uliowekwa. Kihwili alifafanua zaidi kuwa utaratibu huu unazingatia ridhaa ya serikali pamoja na uwezo wa mfuko wa Bima ya Amana katika kufidia wateja.
Akijibu swali la mmiliki wa Full Shangwe Blog, John Bukuku, kuhusu vigezo vilivyotumika kuweka kiwango hicho cha fidia, Kihwili alieleza kuwa kiwango hicho kimewekwa kwa kuzingatia uwezo wa mfuko na hali ya uchumi wa nchi.
“Kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2022, kiwango cha fidia kilikuwa milioni 1.5, lakini kutokana na ukuaji wa uchumi na mfuko kuwa na uwezo wa kifedha zaidi, tumeongeza kiwango hicho mara tano hadi milioni 7.5,” alisema Kihwili.
Pia alisisitiza kuwa si jambo jema kulipa fidia kwa asilimia 100 hata kama mfuko unaruhusu, kwani kuna hofu ya kuibuka kwa tatizo linaloitwa ‘moral hazard,’ ambapo watu hawatakuwa makini katika kufuatilia hali ya benki wanazoweka fedha zao.
Kihwili alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kufuatilia maendeleo ya benki wanazoweka fedha zao kila robo mwaka ili wawe na uhakika wa usalama wa amana zao.