Na Mwandishi Wetu., DAR ES SALAAM
MCHUNGAJI wa Kanisa la Uamsho na Matengenezo ya Kiroho Ulimwenguni, Mwalim Augustine Tengwa amewataka wanasiasa nchini kutumia busara katika maamuzi yao wakati wa uchaguzi kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele ili kuendelea kulinda amani iliyopo.
Lakini pia,amewashauri viongozi wanaofanya maamuzi na kuishauri Serikali kufanya hivyo kwa uaminifu ili kuepuka uchochozi utakaoweza kuliweka Taifa katika hali itakayopelekea uvunjifu wa amani.
Hayo ameyasema leo Oktoba 11,2024 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari amesema upo umuhimu wa wanasiasa kuongozwa na utashi wa ki Mungu katika kufanya maamuzi yao ili kulilinda na kuliokoa Taifa la Tanzania.
“Nivishauri vyombo vya ulinzi na usalama kusimama vema katika nafasi zao ili kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaimarika zaidi kabla na baada ya chaguzi zijazo lakini pia tunapaswa kufanya maombi sana tuliombee Taifa letu lakini tusiache kumuombea zaidi Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan ili Afanye maamuzi sahihi kwa ustawi wa Taifa letu”,Amesema.
Amesema, kutokana na hali hiyo kila Mtanzania analo jukumu la kuhakikisha amani ya nchi inatawala na wanapaswa kuwakemea kiwemo kuwakataa watu au wanasiasa
wachochezi.
Tengwa amesema, Tanzania ni ya Watanzania na hawana taifa mbadala la kukimbilia iwapo wataruhusu wenye nia ovu kutimiza matakwa yao ili kupata nafasi za uongozi.
Kwa upande wake, Nabii Alpha Kiamba amewataka Watanzania kuyapa kisogo maneno na taarifa zenye viashiria vya kuwagawa ambavyo vimekuwa vikizushwa na baadhi ya wanasiasa
wakiwemo wanaharakati mbalimbali.
“Na, suala la upinzani nchini lifanyike katika hekima za Mungu, kwani taarifa zinatolewa ili kuliokoa Taifa na mauti.
“Ndiyo maana tutahitaji watu waombe, kila mkoa watu waingie kwenye maombi.Sasa Mama naye mnampiga mawe usiku na
mchana. Watu wanaokutana na vyombo vya dola na viongozi wake wawe na hekima za kushauri.”
Mchungaji Tengwa akiwa ameambatana na wachungaji wasaidizi katika huduma hiyo yenye makao makuu mkoani Morogoro amesema, kupitia maombi ambayo wamekuwa wakiyafanya mfululizo, Mungu amewaonesha ishara ambayo si njema katika chaguzi zijazo nchini.