Na Sophia Kingimali.
JUMUIYA ya Wafanyabiashara wa Kariakoo(JWK) wamezindua jukwaa la wafanyabiashara na huduma ili kuboresha ustawi wa biashara zao katika soko hilo na kuendelea kulitangaza nje ya mipaka ya Tanzania lakini pia kufungua fursa kwa wafanyabiashara.
Akizungumza leo Octoba 10,2024 wakati akizindua Jukwaa hilo Mwenyekiti wa JWK, Martine Mbwana amesema kuwa wafanyabiashara wa Kariakoo wanakabiliwa na changamoto nyingi na utatuzi wake utafanywa na jukwaa hilo ili kuweza kufanya biashara bila vikwazo vyovyote.
Amesema kuwa pamoja na jitihada za serikali na sekta ya fedha kutoa elimu za upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wafanyabiashara lakini bado ni changamoto kwani hawana taarifa na uwezo wa kupanua biashara zao, kununua bidhaa nyingi kwa bei hafuu, au hata kushindana katika masoko ya kikanda na masoko ya kimataifa.
Pia mbwana amesema kuwa kupata vibali, usafirishaji wa bidhaa, na ushuru, umekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara.
“Soko la Kariakoo limepungua kwa kiasi kikubwa katika ushindani wake
kwenye masoko ya kikanda, hususan katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Biashara za Kariakoo zimekuwa zikikosa uwezo wa kuhimili Ushindani wa wafanyabiashara wa kanda hizi kutokana na changamoto kadhaa”,Amesema.
Amesema Moja ya changamoto hizo ni bei za juu za bidhaa za Tanzania, ambazo zimeathiri uwezo wa kushindana na bidhaa za bei nafuu kutoka nchi jirani. Aidha, urasimu katika taratibu za biashara, hususan katika kupata vibali, usafirishaji wa bidhaa, na ushuru, umekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara wa Kariakoo kufurahia fursa zilizopo kwenye masoko haya ya kikanda.” Ameeleza Mbwana
Akizungumzia siku ya jukwaa hilo, Katibu Mkuu wa Jukwaa la Biashara na Huduma, Fredy Leopold amesema kuwa linatarajiwa kufanyika Novemba 21 hadi 23, 2024 ambapo litawashirikisha zaidi ya watu 900 kutoka ndani na nje ya Tanzania.
“lengo kuu la jukwaa hilli ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi za EAC, SADC na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kukuza ufanisi wa soko la Kariakoo katika biashara za kikanda na kimataifa.”
Amesema jukwaa hilo limeandaliwa kwa kushirikiano wa karibu na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA katika kuhakikisha kuwa ajenda ya maendeleo ya biashara inabebwa na wadau wote kutoka katika sekta ya umma na binafsi.
Amesema kuwa Jukwaa hilo litakuwa la siku tatu litaiwezesha JWK kuitangazia dunia bidhaa na huduma zinazopatikana Kariakoo, mitaa ya Kariakoo na upatikanaji wa huduma pamoja na bidhaa, siku ya pili tutajadiliana huduma zinazorahisisha biashara na siku ya tatu tutajadili mahitaji ya kisekta hasa kuangazia umuhimu wa taaluma na wataalamu katika maendeleo ya Bashara na huduma Kariakoo na nchini kote.
Kwa upande wake Mjumbe wa JWK na mfanyabiashara wa mashuka, pazia na mapambo ya nyumba na ofisini katika soko la Kariakoo, Ida Mwaibula amesema kupitia jukwaa hilo zitatungwa sera mbalimbali ambazo anaamini kuwa zitakazowasaidia katika kufanya biashara zao.