Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza amani na mshikamano kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo. Akizungumza akiwa katika eneo la Tinde, mkoani Shinyanga, Balozi Nchimbi aliwataka Watanzania wote kutanguliza amani kama kipaumbele kikuu katika maisha yao ya kila siku.
Balozi Nchimbi alikumbusha kwamba waasisi wa Taifa walifanya kazi kubwa kuweka misingi ya amani, na ni jukumu la kizazi cha sasa kuhakikisha misingi hiyo inadumishwa. Alisema, “Amani yetu ni msingi wa umoja na mshikamano ambao unapaswa kuendelezwa kwa vizazi vijavyo.”
Aliongeza kuwa ili kudumisha amani, Watanzania wanapaswa kushirikiana, kutatua tofauti kwa njia ya mazungumzo, na kuhakikisha kuwa umoja unalindwa kwa gharama yoyote. “Hatupaswi kukubali kuona umoja wetu ukivurugwa, bali tushirikiane na kuimarisha mazingira ya amani,” alihimiza Nchimbi.
Ziara ya Balozi Nchimbi mkoani Shinyanga inafanyika kwa kushirikiana na viongozi wengine wa CCM akiwemo Katibu wa NEC Itikadi Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdalla Hamid.