Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) imeungana na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuratibu Maonyesho ya Teknolojia ya Madini kwa mwaka 2024, ambayo yameendelea, Oktoba 7, 2024, katila viwanja vya EPZ Bombambili mjini Geita.
Maonyesho haya, yanayofanyika kwa mara ya saba, yanawalenga wafanyabiashara wa madini, Wachimbaji na wadau wengine muhimu katika sekta ya madini.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lucy Mbogoro, Meneja wa Uhusiano wa Umma na Masoko wa TANTRADE, ameeleza kuwa TANTRADE imeanzisha “Kliniki ya Biashara” kwa kushirikiana na taasisi za umma kama SIDO, BRELA, TRA, TMDA, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali na wadau wengine.
Lengo la kliniki hii ni kuwawezesha wafanyabiashara wa madini wa Geita na wengine kutoka maeneo mbalimbali nchini kupata elimu na ushauri unaohusu biashara zao, hususan namna ya kupanua masoko yao hadi kimataifa na kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa.
Mbogoro amesisitiza kuwa kliniki hiyo inalenga pia kutoa majibu kwa maswali na changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa madini.
Kupitia banda la TANTRADE, wafanyabiashara wataweza kujifunza na kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwa wataalam na wadau mbalimbali waliopo kwenye maonyesho hayo.
Aidha, TANTRADE imeanzisha eneo maalum kwenye maonyesho hayo linaloitwa “Made in Tanzania”, ambalo linatenga nafasi kwa wafanyabiashara wanaotengeneza bidhaa za ndani ya nchi.
Eneo hili lina lengo la kuwasaidia wafanyabiashara hao kuonyesha bidhaa zao na kupata fursa za kibiashara ndani na nje ya nchi