Na Neema Mtuka, Rukwa
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Rukwa, Angelina Bidya, amewataka wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuachana na matumizi ya nishati chafu ambayo huathiri mazingira. Bidya alitoa rai hiyo leo, Oktoba 8, 2024, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la maonyesho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja.
Amesema nishati safi, hususan umeme, ina faida nyingi ikiwemo kuokoa muda, kulinda afya, na kuhifadhi mazingira. “Nishati safi inalinda mazingira yetu na pia ni salama kwa afya ya watumiaji,” alieleza Bidya.
Aidha, alihimiza wananchi kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutumia nishati safi ya umeme, hususan kwa kupikia kwa kutumia jiko janja.
“Katika Wiki ya Huduma kwa Mteja, tumejipanga kuhakikisha kuwa kila mteja wetu anapata huduma bora inayostahili, na hivyo kufurahia huduma kutoka TANESCO,” alisema Bidya, akisisitiza kuwa kauli mbiu ya wiki hii ni “Kutoa huduma bora juu na zaidi ya matarajio ya wateja kwa shirika.”
Bidya pia aliongeza kuwa, kupitia wiki hii, TANESCO imepanga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu ulinzi wa miundombinu ya shirika, pamoja na matumizi ya nishati safi ya umeme kwa kupikia.
“Tuungane katika safari ya kutumia nishati safi, kwani matumizi ya umeme kwa kupikia yanahitaji kiasi kidogo cha nishati,” alifafanua Bidya.
Kwa upande wao, baadhi ya wateja wa TANESCO wakiwemo Herman Wikoma, wamesema wanatarajia huduma bora zaidi kutoka TANESCO ili kukidhi matarajio yao.