Na Sophia Kingimali.
VIONGOZI wa Vyama vya siasa nchini (CHAUMA, UPDP, CCK na ACT Wazalendo) wamesema wamejipanga kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu kwa kuridhishwa na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unatumia falsafa ya 4R.
Wakizungumza leo Octoba 7,2024 ofisini kwao baada ya kumpokea Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi, viongozi hao vyama wamesema walikuwa wameshakata tamaa ya kushiriki chaguzi ila kupitia uongozi wa Rais Samia watashiriki na kuibuka na ushindi
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi (CHAUMA), Hashimu Rungwe amesema wanaimani na uongozi wa Rais Samia katika kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo wamejipanga kushiriki kwa nguvu zote kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kuikomboa nchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojole amesema kinaenda kushiriki uchaguzi huo kwa kuwa wanaona nchi inaendeshwa kwa amani na umoja pia ametumia nafasi hiyo kumuomba Rais Samia kuwa vyama vya siasa vinaomba kupata ruzuku ili viweze kuleta ushindani sawa wa kisiasa nchini.
“Msidanganyike wananchi chaguzi zote zijazo zitakuwa huru na haki chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan,”amesema.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi amesema Waziri Lukuvi amekuja na utaratibu mpya na mzuri ambao unaonesha kuviweka pamoja vyama vya siasa nchini.
Aidha Jaji Mutungi amevishukuru vyama vyote 19 vyenye usajili wa kudumu ambavyo vimeonesha nia ya kukutana na Waziri.
“Utaratibu ulioanzishwa na Waziri Lukuvi ni mzuri na unaonesha utawajenga wanasiasa kuwa wamoja kwa lengo la kujenga nchi yetu,”amesema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi amesema ziara hiyo iliyofanywa na Waziri Lukuvi inamanufaa mbalimbali ikiwemo kujua zilipo ofisi za vyama hivyo.
Falsafa ya 4R ya Rais Samia imejikita kwenye Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya.