Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamewahimiza Watanzania, hususan wafanyabiashara, kujitokeza kwa wingi katika banda lao kwenye Maonyesho ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mjini Geita, ili waweze kutatuliwa changamoto zinazohusu usajili wa majina ya biashara, leseni za biashara, na usajili wa kampuni.
Akizungumza leo, Oktoba 5, 2024, alipokuwa Anita maelezo kwa Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Doto Biteko alipotembelea banda la BRELA Afisa Leseni Mwandamizi wa BRELA, Koyan Landway, amesema lengo la taasisi hiyo ni kutoa huduma kwa haraka na kuwapa wananchi elimu kuhusu masuala mbalimbali ya usajili.
“Niwatake wananchi wa Geita na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kwenye banda letu ili kupata huduma na kutatua changamoto zao,” alisema Landway.
Aidha, Landway alibainisha kuwa ushiriki wa BRELA katika maonyesho hayo unalenga kuwafikia wadau wao, hususan wafanyabiashara waliopo kwa wingi katika maonyesho hayo, ili waweze kutangaza biashara zao na kupata huduma zinazotolewa na BRELA.
Maonyesho hayo ya Teknolojia ya Madini yanafanyika katika viwanja vya EPZ Bombambili, mjini Geita.