Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo (Mb), ameagiza Bodi mpya ya Tume ya Ushindani (FCC) kuhakikisha wanachukua hatua za haraka katika kuimarisha ushindani wa kibiashara nchini, kwa kuweka mbele maslahi ya umma na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha ajira. Waziri Jafo alisisitiza umuhimu wa kuharakisha vikao vya bodi na kushughulikia changamoto za kibiashara kwa lengo la kuchochea ajira, wakati akizindua rasmi bodi hiyo Oktoba 4, 2024, jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia nafasi ya FCC katika maendeleo ya kiuchumi, Mhe. Jafo alisema taasisi hiyo ina jukumu kubwa la kusaidia nchi kufikia malengo ya ukuaji wa uchumi kupitia uwekezaji. Alisema, “Taasisi hii ni muhimu kwa kuhakikisha ushindani wenye tija, ambao utafungua nafasi za ajira na kuchochea uwekezaji nchini.” Waziri aliagiza kwamba kampuni zinazotaka kuungana zisaidiwe kwa haraka, huku taratibu zote za kisheria zikifuatwa, ili kuokoa na kuongeza ajira kwenye makampuni hayo.
Waziri Jafo pia aliwahimiza wataalam wa FCC kutoa ushirikiano kwa bodi ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu yao kwa ufanisi. “Ninyi ni injini ya utendaji wa taasisi hii. Ushirikiano wenu na bodi utawezesha kazi kufanyika kwa maslahi mapana ya taifa na kuinua uchumi wetu,” aliongeza.
Katika kikao hicho, Mhe. Jafo aliwakumbusha wajumbe wapya wa bodi kuweka mbele uwajibikaji, waadilifu, na kuepuka maslahi binafsi. Alisisitiza umuhimu wa kuishi kwa mshikamano na kufanya kazi kama timu moja, ili kuleta mafanikio kwa taasisi na kwa taifa kwa ujumla.
Bodi hiyo imezinduliwa baada ya uteuzi wa wajumbe watatu wapya: Bw. Said Habibu Tunda kutoka Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Prof. Jehovaness Aikael kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na CPA. Dkt. Shufaa M. Al-Beity kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM).