Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, amesisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa NHC Mkoa wa Lindi kuongeza bidii na kujituma ili kuhakikisha Shirika linaendelea kutoa huduma bora kwa Watanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa taifa kupitia gawio kwa serikali.
Bw. Abdallah alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa NHC Lindi wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi pamoja na utendaji wa Shirika hilo mkoani humo.
Katika mazungumzo yake, Mkurugenzi Mkuu alieleza kwamba Shirika linawategemea wafanyakazi wake kwa kiwango kikubwa, na hivyo ni muhimu kwao kuzingatia maadili ya kazi, kuongeza ufanisi, na kuhakikisha miradi ya ujenzi inakamilika kwa viwango vya juu. Aidha, alibainisha kuwa Menejimenti ya NHC itaendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi pamoja na mazingira ya kazi ili kuwawezesha wafanyakazi kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Bw. Abdallah pia aliwahimiza wafanyakazi kushirikiana na Menejimenti katika kutekeleza malengo ya Shirika kwa lengo la kujenga nyumba bora kwa ajili ya wananchi na kuongeza tija inayotokana na miradi ya ujenzi.
Alisisitiza kuwa hatua hizo zitapelekea NHC kuwa na uwezo wa kuchangia zaidi katika maendeleo ya taifa kupitia gawio kwa serikali.
Kwa upande wao, wafanyakazi wa NHC Lindi waliipongeza Menejimenti kwa jitihada zake za kuboresha maslahi yao, wakiahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuleta mafanikio zaidi kwa Shirika.
Pia walionyesha kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Menejimenti katika kuboresha mazingira yao ya kazi, jambo ambalo limeongeza ari na mori wa utendaji kazi miongoni mwao.
Mkurugenzi Mkuu wa NHC Bw. Hamad Abdallah akikagua ujenzi wa jengo kubwa na la kisasa linajengwa na NHC eneo la Mtanda Lindi kwa ajili ya Ofisi na shughuli za kiabiashara. Anayetoa maelezo kwa Mkurugenzi Mkuu ni Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC QS Dkt Godwin Maro na pia yupo Meneja wa NHC Mkoa wa Lindi Bw. Omari Makalamangi.