DC Same Awataka Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Kujiepusha na Rushwa
Ashrack Miraji – Fullshangwe Media, Kilimanjaro
Mkuu wa Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni, amewataka wasimamizi na wasaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2024 kujiepusha na vitendo vya rushwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Ameonya kuwa rushwa ni adui wa haki na husababisha kudumaa kwa maendeleo ya jamii.
Akizungumza wakati wa kufungua semina ya mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi huo, inayotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024, DC Kasilda alisisitiza umuhimu wa kufuata miongozo na kanuni zilizotolewa na Wizara ya TAMISEMI kwa Halmashauri.
“Hii ni kazi maalum ambayo mnaenda kuitekeleza, mnawaongoza wananchi. Niwaombe sana, epukeni masuala ya rushwa. Rushwa ni adui wa haki na hudumaza maendeleo. Kanuni za utumishi wa umma zinakataza mtumishi kujihusisha na rushwa au mambo yanayoshusha hadhi ya mtumishi wa umma,” alisema DC Kasilda.
Pia, aliwaagiza watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha kuwa wanawahamasisha wananchi ipasavyo kuhusu ratiba na matukio ya uchaguzi, kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kufikisha taarifa za serikali, huku wakizingatia maslahi ya taifa.