Moroni, Comoro
Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu, amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uagizaji Mchele nchini Comoro (ONICOR), Moussa Hamada, ambapo walijadili namna bora ya kuongeza uagizaji wa mchele kutoka Tanzania.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ubalozi wa Tanzania jijini Moroni, Balozi Yakubu alieleza kuwa Tanzania ni chaguo bora kwa Comoro katika kuagiza mchele kutokana na ukaribu wa kijiografia, ubora wa mchele wa Tanzania, urahisi wa upatikanaji, pamoja na idadi kubwa ya mavuno inayoongezeka kila mwaka nchini humo.
Aidha, Balozi Yakubu alibainisha kuwa makongamano ya hivi karibuni yameonyesha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa mchele nchini Comoro na changamoto kadhaa zinazohitaji kufanyiwa kazi kati ya Mamlaka ya ONICOR na wadau wa nje. Mazungumzo hayo yalilenga kutafuta suluhu ya changamoto hizo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa ONICOR, Moussa Hamada, alieleza kuwa ni wakati mwafaka kujadili suala hilo kwa kina kutokana na umuhimu wa mchele, ambao ni chakula kikuu kwa wananchi wa Comoro. Alibainisha kuwa mahitaji ya mchele kwa visiwa vyote vya Comoro ni tani 300-350 kwa siku.
Balozi Yakubu alitumia fursa hiyo kumkaribisha Bwana Hamada kutembelea Tanzania ili kuona maeneo ya uzalishaji wa mchele na kuonana na wadau muhimu kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano katika sekta hiyo muhimu.