Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul, amepongeza uongozi wa Chuo cha Ufundi Furahika (VETA) kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kila kijana wa Kitanzania anapata elimu itakayomwezesha kujiajiri au kuajiriwa, bila kujali hali yake ya kipato.
Pongezi hizo zilitolewa leo, Septemba 28, 2024, jijini Dar es Salaam, wakati wa mahafali ya 16 ya chuo hicho, ambapo wanafunzi 220 walihitimu masomo yao katika fani mbalimbali.
“Nampongeza Rais wetu, Dkt. Samia, kwa kutoa fursa hizi za elimu, na pongezi pia kwa Mkuu wa Chuo hiki kwa kufanikisha mpango wa kuwawezesha vijana waliokosa fursa ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha au sababu nyinginezo. Hawa vijana sasa wanapata elimu bila malipo yoyote,” alisema Waziri Anna Athanas.
Aliendelea kwa kusisitiza kwamba jitihada zinazofanywa na uongozi wa chuo hicho kutoa elimu bure ni mfano wa kuigwa. “Ni matumaini yangu kwamba wadau wengine watafuata nyayo hizi kwa kuwaendeleza vijana kielimu, ili waweze kujiajiri na kuachana na utegemezi wa ajira za serikali ambazo hazitoshi kwa wote,” aliongeza.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Elias Mpanda, pia aliwasihi wazazi kupeleka vijana wao chuoni hapo ili wapate elimu bure na kutumia fursa ya Rais Samia katika kuwaendeleza vijana wa Kitanzania, hususan wale waliokosa nafasi ya kuendelea na masomo kutokana na changamoto za kifedha.
“Mbali na hilo, naomba wadau mbalimbali waiunge mkono serikali kwa kusaidia chuo hiki kwa vifaa vinavyohitajika kama vile cherehani, kompyuta, na vinginevyo. Hii itasaidia vijana wengi kujiendeleza na kujiepusha na makundi maovu,” alisema Mpanda.
Naye Mkuu wa Chuo, Dkt. David Msuya, alieleza kuwa kati ya wanafunzi 220 waliomaliza masomo, wengi wao tayari wamepata ajira, hasa baada ya kufanya mafunzo kwa vitendo (‘field’). “Sina shaka na wahitimu hawa, wengi wao tayari wameajiriwa Zanzibar, Arusha, na Dar es Salaam. Wengine watakosa ajira serikalini lakini wataweza kujiajiri kwa uwezo walio nao,” alisema Dkt. Msuya.
Aliongeza kuwa kila mwaka chuo kinapanga kupokea wanafunzi kati ya 400 hadi 500, ingawa idadi hiyo haifikiwi kutokana na changamoto za wazazi kushindwa kupeleka watoto wao chuoni. Aliwahimiza wazazi kupeleka vijana wao kwa ajili ya masomo katika muhula mpya, huku akisisitiza kuwa ada pekee itakayolipwa ni ya mtihani wa serikali, ambayo ni shilingi 50,000 tu.