Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Bw. Hamad Abdallah, amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, mkoani Mbeya, kukagua nyumba za gharama nafuu zilizojengwa na shirika hilo kwa ajili ya watumishi wa serikali. Nyumba hizo ni sehemu ya jitihada za NHC kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapata makazi bora na yenye gharama nafuu, ili kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wananchi.
Akipokelewa na Meneja wa NHC Mkoa wa Mbeya, Bw. Erasto Chilambo, Mkurugenzi Abdallah alielezea kuridhishwa kwake na mradi huo, ambao unalenga kuboresha maisha ya watumishi na kupunguza changamoto za makazi, hususan kwa watumishi wa serikali katika maeneo ya vijijini. “Ninafuraha kuona kuwa nyumba hizi zimejengwa kwa viwango bora na kwa gharama nafuu, na zinaleta tija kwa watumishi wa serikali ambao kwa muda mrefu wamekuwa na changamoto za makazi,” alisema Bw. Abdallah.
Bw. Hamad Abdallah alisisitiza kuwa NHC itaendelea kushirikiana na halmashauri na taasisi mbalimbali nchini kuhakikisha miradi ya ujenzi wa nyumba bora inaendelea kote nchini, hususan katika maeneo yenye uhaba wa makazi ya watumishi. “Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ni mfano mzuri wa namna tunavyoweza kushirikiana na serikali za mitaa katika kuhakikisha watumishi wanapata makazi bora. Tunataka kuona miradi kama hii ikienea nchi nzima,” aliongeza.
Katika ziara hiyo, Bw. Abdallah pia alipata fursa ya kutembelea miradi mingine ya ujenzi inayosimamiwa na NHC mkoani Mbeya, ikiwemo ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa ajili ya wananchi wa kipato cha chini. Miradi hiyo inalenga kupunguza tatizo la makazi na kuongeza upatikanaji wa nyumba bora katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu aliahidi kuwa NHC itaendelea kushirikiana na wadau wengine ili kuhakikisha miradi ya nyumba za gharama nafuu inakidhi mahitaji ya jamii, huku akisisitiza umuhimu wa usimamizi mzuri wa rasilimali za shirika.
Aliongeza kuwa Shirika la Nyumba la Taifa lina mipango ya kupanua miradi yake ya ujenzi wa nyumba katika mikoa mingine ya Nyanda za Juu Kusini, ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.