Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mkoani Kilimanjaro, Anne Kilango Malecela, amezindua rasmi shina la Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) katika kijiji cha Kadando, Kata ya Maore, wilayani Same.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mheshimiwa Kilango aliwasihi vijana kuendelea kufanya kazi kwa umoja, huku wakidumisha mshikamano ili kulinda heshima ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kusambaza ujumbe wa mafanikio ya serikali kwa wananchi.
“Vijana ni nguzo muhimu katika maendeleo ya nchi. Ni vyema mkaendelea kushikamana na kulinda amani yetu. Epukeni makundi chonganishi yenye nia mbaya kwa taifa,” alisema Kilango.
Mbunge huyo pia alieleza furaha yake kwa vijana kwa hatua waliyochukua ya kuanzisha shina hilo. “Mheshimiwa Rais wetu atafurahi sana akiona jambo hili. Nyie ni nguzo muhimu ya taifa letu, na mmeheshimisha Chama cha Mapinduzi. Nitaendelea kuwaunga mkono kwa asilimia mia moja. Endeleeni kuleta vijana zaidi katika umoja huu,” aliongeza.
Awali, Mwenyekiti wa UVCCM Tawi la Kadando, Hosseni Mussa, aliwasilisha taarifa ya ujenzi wa shina hilo. Alisema kuwa umoja wao umefanikiwa kuwaunganisha vijana wote, na sasa wote ni makada wa CCM. Vijana hao walimpongeza Mbunge Kilango kwa kazi kubwa anayofanya kwa maendeleo ya wananchi wa jimbo hilo.
Katika uzinduzi huo, Mheshimiwa Anne Kilango Malecela alichangia shilingi laki tano kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya vijana wa UVCCM.