Na Mwandishi Wetu, NCAA.
Zoezi la kuelimisha wananchi kuhama kwa hiari ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro limeendelea kueleweka ambapo leo tarehe 28 Septemba 2024 kaya 28 zenye watu 130 na mifugo 346 zimehama kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda Kijiji cha Msomera Wilaya ua Handeni na Makao Wilaya ya Meatu
Kwa mujibu wa kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi (Idara ya Maendeleo ya jamii) Gloria Bideberi kati ya kaya 28 zilizohama leo, kaya 26 zenye watu 119 na mifugo 329 zimehamia kijiji cha Msomera Handeni na Kaya 2 zenye watu 11 na mifugo 17 zimehamia kijiji cha Makao Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Ameongeza kuwa tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni 2022 hadi kufikia tarehe 28 Septemba, 2024 Jumla ya kaya 1,655 zenye watu 9,976 na mifugo 40,397 zimeshahama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.
Kamishna Bideberi amefafanua kuwa kwa sasa wananchi wanaojiandikisha kuhama kwa hiari zoezi ni la muda mfupi ambapo kila kaya zinazojiandikisha zinahamishwa katika muda wa wiki mbili.
“Serikali imeendelea kuwezesha zoezi hili ndio maana mnaona hata tukipata kaya chache zinazojiandikisha hatuna haja ya kuwasubirisha mda mrefu, tunawahamisha kwa haraka wakati wengine wakiendelea kujiandikisha kwa kuwa zoezi hili ni endelevu na linafanyika kwa umakini mkubwa” ameongeza Bideberi.
Akiaga kundi hilo kwa niaba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori Dkt. Alex Lobora amewapongeza wananchi wote wa Ngorongoro kwa kuendelea kuhama kwa hiari kwa ajili ya kupisha na kuimarisha shughuli za uhifadhi lakini pia kuboresha Maisha yao katika maeneo bora zaidi na salama nje ya Hifadhi.
Dkt. Lobora amebainisha kuwa uamuzi wa wananchi hao kuhama unaashiria matokeo chanya ya kuiokoa hifadhi ya Ngorongoro kwa maslahi ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa kuwa Ngorongoro ni eneo la urithi wa dunia ambalo kutokana na uhifadhi endelevu limeendelea kuvutia watalii wengi na Serikali kupata mapato yanayoiwezesha kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Ngorongoro na Watanzania kwa ujumla.
‘Nawasihi muendelee kuwa mabalozi katika kushawishi ndugu zenu waliobaki ili nao wahame kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uhifadhi wa Wanyamapori, mazingira, misitu, malikale na ikolojia ya Ngorongoro ambayo tunaamini uhai endelevu wa Ngorongoro unazinusuru pia hifadhi za maeneo ya jirani inazopakana nazo” aliongeza Dkt. Lobora.
Kwa upande wake mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi NCAA, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Lilian Magoma
amesema hatua ya Wananchi kuhama ndani ya hifadhi imezingatia ushirikishwaji kwa kuwaelimisha umuhimu wa kupisha shughuli za hifadhi katika eneo la Ngorongoro ili wananchi waweze kujiendeleza katika Maisha bora zaidi na salama nje ya hifadhi.
“Wananchi walio wengi wanatambua kuwa sheria za uhifadhi zinakataza baadhi ya shughuli za kiuchumi kufanyika kama ujenzi wa nyumba za kudumu, Kulima, kuingiza umeme, kumiliki vyombo vya moto, na kuamua kuhama kwenda maeneo mengine, Serikali tutaendelea kuimarisha uhusiano na wananchi wa Ngorongoro na kuhakikisha tunawashirikisha katika kila hatua ya utekelezaji wa mpango wa kuhama kwa hiari kwa ajili ya kupisha shughuli za uhifadhi na kuimarisha ustawi wa Maisha yenu” amefafanua Magoma
Magoma amehitimisha kwa kueleza kuwa wananchi wanaohama ndani ya Hifadhi wametengewa eneo la kutosha kwa ajili ya malisho ambao Kijiji cha Msomera kuna hekta 22,000, Kijiji cha Saunyi hekta 9,000 na Kijiji cha kitwai hekta 53,000 za malisho hali inayotosheleza malisho kwa mifugo ya Wananchi wanaoendelea kuhamia maeneo hayo.