………………
Happy Lazaro,Arusha .
Arusha.Walimu nchini wametakiwa kutumia mbinu shirikishi katika kuwafundisha wanafunzi masomo ya sayansi kwa vitendo zaidi ili waweze kuhamasika kusoma masomo hayo.
Hayo yamesemwa na Mdhibiti Mkuu ubora wa shule ya Meru,Aurelia Kiwale wakati akizungumza katika mahafali ya nne ya darasa la Saba katika shule ya mchepuo wa kiingireza ya Silverleaf Academy ambapo jumla ya wanafunzi 45 wamehitimu masomo yao.
Kiwale amesema kuwa,ni wajibu wa walimu kuhakikisha wanatumia mbinu shirikishi ambazo zitawawezesha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi kwani wengi wanakwepa masomo hayo kutokana na mbinu zinazotumika na hivyo kuona masomo hayo ni magumu.
“Mnatakiwa mhamasishe wasichana kupenda masomo ya sayansi kwani ulimwengu wa sasa hivi bila kuwa wasomi waliobobea kwenye maswala ya sayansi ni changamoto kubwa kwani dunia ya sasa hivi inaenda na sayansi na teknolojia kulingana na mabadiliko yalivyo hivi sasa.”amesema .
Aidha amewataka walimu kutoka shule mbalimbali kuhakikisha wanafundisha kwa moyo somo hilo la sayansi ikiwa ni pamoja na kutumia njia mbalimbali za kufundishia ili waweze kulielewa somo hilo na kulipenda .
Amesema kuwa,wamekuwa wakihakikisha sheria na taratibu za utoaji elimu nchini zinasimamiwa na zinazingatiwa mwa kutembelea taasisi, shule za msingi, sekondari na hata vyuo .
Kwa upande wake Mwalimu Pascaline Sarakikya kutoka shule hiyo ya Silverleaf Academy, amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri katika masomo yao huku wakiandaa watoto kuweza kujitegemea kwa kuwafundisha somo la ujasiriamali kwa vitendo ikiwemo namna ya kushona na kutengeneza keki .
Sarakikya amesema kuwa,wamekuwa wakifundisha stadi za maisha na kuweza kuwaandaa wanafunzi hao kuweza kujitegemea pindi watakapomaliza yao kwa kuweza kuweka bustani ndogondogo pamoja na kujifunza kutengeneza keki kwa ajili ya biashara na hata kushona mikoba na hivyo kuweza kujiajiri badala ya kukaa bila ya kuwa na shughuli yoyote.
“Sisi tumejikita kwenye maswala ya teknolojia zaidi tunataka kuhakikisha kuwa watoto wanatumia teknolojia na kujifunza zaidi ili waweze kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwani tunatumia njia mbalimbali kuhakikisha elimu inaboreshwa.”
Mmoja wa wanafunzi waliohitimu masomo shuleni hapo ameushukuru uongozi wa shule hiyo kwa namna ambavyo umewafundisha kuweza kujitegemea pindi watakaporudi majumbani na hata kuweza kujipatia kipato.
“Kwa kweli tunaishukuru shule hii kwa namna ambayo imekuwa ikitufundisha masomo mbalimbali kwa vitendo kwani hivi sasa tunaweza kutengeneza mikate, kushona nguo,pamoja na namna ya kulima bustani ndogo ndogo.”wamesema wanafunzi hao.