Na Fauzia Mussa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezindua vitalu viwili vipya vya uwekezaji wa mafuta na gesi asilia katika maeneo ya nchi kavu, hatua inayolenga kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali katika hafla iliyofanyika hoteli ya Verde, Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Shaaban Ali Othman, alisema uzinduzi huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050, Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025, Mpango wa Maendeleo ya Zanzibar (ZADEP 2021-2026), pamoja na Sera ya Uchumi wa Buluu ya mwaka 2022.
Waziri Othman alieleza kuwa vitalu hivyo vipo katika maeneo ya Unguja na Pemba, na kwamba hatua hii inalenga kuendeleza juhudi za utafutaji wa nishati ya mafuta na gesi asilia kwa kushirikiana na makampuni ya kimataifa ya mafuta na gesi asilia (IOCs).
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inatarajia kupata makampuni mengi ya uwekezaji yatakayojihusisha na utafutaji na uchimbaji wa nishati hiyo, kwa lengo la kuhakikisha rasilimali hizi zinatumika kwa njia endelevu.
Waziri aliwasihi wawekezaji wenye nia ya kuwekeza katika sekta hiyo kuwasilisha maombi yao ili kuingia mikataba ya uwekezaji ndani ya vitalu hivyo.
Vilevile, alikumbusha kuwa duru ya kwanza ya utoaji wa vitalu nane vya baharini kwa kampuni za utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi ilizinduliwa mwezi Machi mwaka huu.
Katika mkutano huo, Wizara hiyo pia ilizindua namba mpya za mawasiliano ya moja kwa moja, 0652630048 na 0652630084, ambazo wananchi wanaweza kutumia kutoa taarifa au kueleza changamoto wanazokutana nazo katika huduma zinazotolewa na Wizara hiyo.