Na Sophia Kingimali
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya kwanza ya wanafunzi watakaonufaika na mikopo kwa mwaka wa masomo wa 2024/2025, ambapo imeongezeka kwa asilimia 5.
Aidha, vyuo ambavyo bado havijawasilisha matokeo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo vimetakiwa kufanya hivyo haraka ili malipo yao yaandaliwe bila kuchelewa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Septemba 28, 2024, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema orodha hiyo ya awamu ya kwanza inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa vyuo vikuu, wanafunzi wa Shule ya Sheria kwa Vitendo, na wanafunzi wa shahada za uzamili. Jumla ya wanafunzi 21,509 wataanza kupokea mikopo, ambayo itagharimu shilingi bilioni 70.78.
“Leo tumeanza kutoa taarifa za mikopo kwa makundi yote ya wanafunzi. Wapo ambao maombi yao bado yanafanyiwa kazi, lakini kila mwombaji atapata taarifa kupitia akaunti yake ya mtandao aliyoitumia kuomba mkopo, bila kuhitaji kufika ofisi za HESLB,” alisema Dkt. Kiwia. Aliongeza kuwa upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada na shahada ya uzamivu bado unaendelea.
Pia, Dkt. Kiwia amesisitiza kuwa bodi hiyo tayari imeanza kuandaa malipo kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo, lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zinafika vyuoni kwa wakati. Aliwataka wakuu wa vyuo kuharakisha kuwasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi ili kuepuka ucheleweshaji wa malipo.
“Kuna baadhi ya vyuo ambavyo havijawasilisha matokeo ya mitihani ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo. Tumewakumbusha waharakishe ili tuweze kukamilisha malipo kwa wakati,” alisema Dkt. Kiwia.
Wanafunzi waliopangiwa mikopo watapata taarifa hizo kupitia akaunti zao za mtandao zijulikanazo kama ‘SIPA’ (Student’s Individual Permanent Account). Kupitia akaunti hizo, wanaweza kuangalia taarifa zote za mikopo kwa njia ya simu au kompyuta.
Akizungumzia bajeti ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025, Dkt. Kiwia alisema serikali imetenga shilingi bilioni 787 kwa ajili ya wanafunzi 245,799, wakiwemo zaidi ya wanafunzi 88,000 wa mwaka wa kwanza ambao wametengewa shilingi bilioni 284.8. Bajeti hiyo imeongezeka kwa shilingi bilioni 38, sawa na asilimia 5, ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa masomo 2023/2024 ambayo ilikuwa bilioni 749.
Aidha, Dkt. Kiwia alieleza kuwa elimu iliyotolewa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini kuhusu namna ya kuomba mikopo imesaidia kupunguza makosa ya waombaji, hivyo kuharakisha mchakato wa kupokea mikopo.
Kwa upande wake, Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu na vya Kati (TAHLISO), Bi. Zainab Kitima, ameishukuru serikali kwa jitihada zake za kuongeza mikopo kutoka shilingi 200,000 hadi 530,000, akisema kuwa ongezeko hilo limepunguza mzigo kwa wazazi na wanafunzi, hasa kutoka familia zenye hali duni.
“Tunaishukuru sana serikali. Leo tumemsikia Mkurugenzi Dkt. Kiwia akisema mikopo itafikishwa vyuoni kwa wakati, jambo ambalo ni faraja kwa wanufaika wa mikopo kote nchini. Hata hivyo, tunaendelea kutoa wito kwa HESLB kuzingatia changamoto zingine ambazo bado tunazo,” alisema Zainab.
Orodha ya awamu ya pili ya wanafunzi watakaopata mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025 inatarajiwa kutangazwa wiki ijayo.