Na John Bukuku- Fullshangwe Media
Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa agizo kwa taasisi zote za umma kuhakikisha zinafuata matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma kwa kutumia Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha thamani halisi ya fedha za umma inapatikana.
“Nimesikia kuwa zipo baadhi ya taasisi nunuzi bado zinasitasita kutumia Mfumo wa NeST ingawa zimewezeshwa kuutumia. Nazielekeza taasisi zote za umma kuzingatia matakwa ya sheria ya ununuzi wa umma na kutumia Mfumo wa NeST ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha tunapata thamani halisi ya fedha. Na endapo watakuwa na changamoto yoyote wanapaswa kuwasiliana na PPRA ili wapate maelekezo na idhini ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa,” amesema Dkt. Nchemba.
Akihutubia wakati PPRA alipokabidhiwa ripoti ya utendaji kazi wa taasisi hiyo kwa mwaka 2023/2024 mbele ya Mwenyekiti wa PPRA, Waziri Nchemba ameeleza kuwa sheria imeweka bayana kwamba kufanya ununuzi nje ya mfumo wa kielektroniki ni kosa la jinai. Alionya kuwa mtu yeyote atakayebainika kufanya hivyo kwa makusudi atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kifungo cha miaka mitatu jela.
Waziri Nchemba ameelekeza PPRA kuendelea kutoa mafunzo kwa watumiaji wa mfumo wa NeST ili kuhakikisha kuwa watumiaji wote wanauelewa wa kutosha wa mfumo huo. Aidha, aliagiza nguvu zaidi zielekezwe katika kutoa elimu kwa umma na uhamasishaji ili Watanzania waweze kufahamu, kuunga mkono, na kujisajili kama wazabuni kushiriki kwenye michakato ya ununuzi wa umma.
“Hii ni muhimu kwa kuwa fursa za upendeleo zilizotolewa na Sheria ya Ununuzi wa Umma kwa Watanzania haziwezi kupatikana kama hawatakuwa wamejisajili kwenye Mfumo huu wa NeST,” amesema.
Dkt. Nchemba pia amegusia changamoto nyingine, akieleza kuwa baadhi ya taasisi bado hazitengi asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa makundi maalum kama inavyotakiwa na sheria. Alisema kuwa kitendo hiki kinaathiri juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwainua Watanzania wote, hususan wale wa hali ya chini, wakiwemo wanawake, vijana, wazee, na watu wenye ulemavu.
“Makundi haya yanapata fursa kwa kujiunga kwenye vikundi vya watu 5 hadi 20, wanafuata utaratibu na kuomba zabuni zilizotengwa kwa ajili yao. Nazielekeza taasisi nunuzi kuzingatia sheria na kuunga mkono juhudi hizi za kuwainua Watanzania wenzetu ili washiriki keki ya Taifa,” amesema Waziri Nchemba.
Ameendelea kuhimiza PPRA kuendelea kutoa elimu kwa umma, ili makundi maalum yaongezeke na wananchi wafahamu jitihada za serikali za kuwafikishia fursa na kuzalisha ajira.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Nchemba ameelekeza Bodi na Menejimenti ya PPRA kuhakikisha mafanikio yaliyopatikana yanadumishwa. Alisisitiza umuhimu wa kudumisha misingi ya uadilifu, uwajibikaji, na kufuata sheria ili kujenga taasisi yenye tija na heshima katika bara la Afrika.
“Napenda tuone ukuaji wa taasisi hii kila mwaka ili kuwapa ahueni watoa huduma na wananchi kwa ujumla,” amehitimisha Waziri Nchemba.