Mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Bi Pendo Mangali wakati akitoa maelekezo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27 /2024.
Msimamizi wa uchaguzi katika wilaya ya Kalambo Shafi Mpenda wakati akitoa maelekezo ambayo ndio mwongozo wa uchaguzi wa Serikali za mitaa.
…………….
Rukwa
Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Bi. Pendo Mangali, ametoa maelekezo kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024. Maelekezo hayo yalitolewa leo, Septemba 27, 2024, kwenye mkutano uliowashirikisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, siasa, wananchi na makundi yote ya jamii.
Bi. Pendo amewahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Mpiga Kura.
Aidha, amewataka washiriki katika kugombea na kuchagua viongozi watakaosaidia kuleta maendeleo katika jamii.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo wameahidi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujiandikisha na kuhakikisha wanachagua viongozi wenye hekima na uwezo wa kuleta maendeleo. Mchungaji Imani Mwansope aliunga mkono wito huo akisisitiza kuwa elimu ya kupiga kura ni muhimu ili jamii iweze kuchagua viongozi bora.
“Wananchi wakiwa na elimu kuhusu uchaguzi wataweza kuchagua viongozi wa kweli, siyo wababaishaji,” alisema Mwansope.
Pia, Bi. Pendo aliwakumbusha wananchi kuwa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ni hatua muhimu inayompa kila mwenye sifa haki ya kisheria kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea.
Wakati huohuo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Kalambo, Shafi Mpenda, ametangaza rasmi tarehe ya uchaguzi na kuwataka wadau wa uchaguzi kuwafikia makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, kwa kutoa elimu juu ya ushiriki wao.
Mpenda alibainisha kuwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 571, uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba 2024, na zoezi la uandikishaji wapiga kura litafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba 2024 katika vituo vilivyopangwa.
Alieleza kuwa maelekezo hayo yanalenga kutoa mwongozo wa wazi na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na usawa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa.