Septemba 26, 2024
Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, ametoa wito kwa wananchi wenye umri wa kuanzia miaka 21 kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa na wajumbe wa mtaa ifikapo Novemba 1 hadi 7, 2024.
Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, na wadau wengine kuwa mabalozi wa kuhamasisha jamii kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, zoezi litakalofanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu.
Akizungumza katika kikao maalum cha kutoa maelekezo kuhusu uchaguzi huo, Dkt. Shemwelekwa alisisitiza, kila mwananchi mwenye umri wa miaka 18 ana haki ya kupiga kura lakini sifa ya mgombea kuanzia miaka 21.
Kwa mujibu wa tangazo la Serikali Namba 574 la Julai 12, 2024, uchaguzi wa viongozi wa mtaa utafanyika Novemba 27, baada ya uandikishaji wa wapiga kura.
Dkt. Shemwelekwa alifafanua, uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8, ambapo fursa ya kuweka pingamizi itawekwa wazi kati ya Novemba 8 na 9, huku rufaa dhidi ya uteuzi zikitarajiwa kuwasilishwa kuanzia Novemba 10 hadi 13 huku kampeni rasmi zikitajwa kuanza Novemba 20 hadi 26.
Kwa upande wake, Ofisa wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, Mwanyika Senzota, aliwaasa wananchi kuchagua wagombea waadilifu na kupinga rushwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo, alihakikisha kuwa jeshi la polisi limejipanga kudumisha amani wakati wote wa uchaguzi, akisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja hata baada ya uchaguzi.
“Amani ni ya muhimu zaidi, tofauti zetu zisituharibie amani,” alisema Lutumo.