Msimamizi wa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda, amewasihi wadau wa uchaguzi kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Akizungumza kwenye kikao cha kutoa maelezo ya uchaguzi kwa wadau hao, Bieda alitoa ratiba nzima ya uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024. Alisema zoezi la kuandikisha wapiga kura litafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 20 Novemba 2024, likifuatiwa na zoezi la kubandika orodha ya wapiga kura tarehe 21 Novemba 2024.
Wadau walioshiriki kwenye kikao hicho ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, watu wenye ulemavu, wazee maarufu, viongozi wa ulinzi na usalama, na wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya wilaya.
Aidha, amesema kuwa kampeni za uchaguzi huo zitaanza tarehe 20 hadi 26 Novemba 2024, na uchaguzi utafanyika tarehe 27 Novemba 2024. Bieda amewahakikishia wadau hao kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa katika Halmashauri hiyo utafanyika kwa uhuru na haki.
Afisa Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kibaha Grace Haule amewataka wadau mbalimbali kuhamasisha jamii kutoka makundi mbalimbali kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na hatimaye kupiga kura katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.
Kwa upande wao, wadau na viongozi walioshiriki kikao hicho, wakiwemo masheikh, wamewasihi wanasiasa kuhimiza amani na uzalendo kwa kuweka maslahi ya nchi mbele, kwani kuna maisha baada ya uchaguzi.
Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ina jumla ya vijiji 26 na vitongoji 102 vitakavyoshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2024.