Na Ashrack Miraji, Fullshangwe Media
Mbunge wa Jimbo la Lushoto, Mhe. Alhaj Shabani Omary Shekirindi, amewasihi wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba mwaka huu.
Mhe. Shekirindi alitoa wito huo wakati wa hadhara ya Maulid iliyoandaliwa na wanawake wa Kata ya Mlola, Kitongoji cha Hondelo, wilayani Lushoto, mkoani Tanga.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza akina mama wa kitongoji hiki kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya. Pia niwaombe akina mama na wananchi wote kwa ujumla kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Chagueni viongozi bora wenye maslahi ya taifa letu na maendeleo ya jamii. Tuwakatae viongozi wanaotoa rushwa kwa maslahi binafsi,” alisema Mhe. Shekirindi.
Aidha, alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa za kuleta maendeleo nchini. “Leo tunashuhudia ujenzi wa barabara kubwa na ya kisasa, ambayo itasaidia sana kuboresha huduma za kijamii na kufungua fursa za kiuchumi katika kata hii. Hii ni kazi ya Rais wetu, na ni kwa ajili ya wananchi, hususani kina mama na wafanyabiashara,” aliongeza.
Mbunge huyo pia alizungumzia maendeleo ya jimbo lake, akibainisha kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara, anayofanya juhudi kubwa kuhakikisha umeme unafika katika vijiji ambavyo bado havijaunganishwa ndani ya jimbo hilo.
“Mimi kama Mbunge wenu, naendelea kupambana kwa hali na mali. Barabara ambayo ilikuwa kero kwa muda mrefu sasa inakaribia kukamilika, itawaunganisha kata na vijiji. Sasa napambana kuleta umeme kwa wakazi wa vijiji ambavyo vipo kwenye jimbo langu,” alisema.
Pia, Mhe. Shekirindi alitoa onyo kali kwa baadhi ya viongozi wanaodai ujenzi wa barabara hiyo unafanyika kwa nguvu zao binafsi, akiwataka wananchi kuwa makini na taarifa za kupotosha zinazotolewa na viongozi hao.