Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufiani wakibadilishana hati za makubaliano ya mpango maalum wa mikopo kwa wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub na Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufiani wakisaini hati za makubaliano ya mpango maalum wa mikopo kwa wafanyabiashara.
………………
Benki ya Equity imeanzisha mpango maalum wa mikopo kwa wafanyabiashara wanaosambaza bidhaa za kampuni ya Bakhresa, ambapo sasa wanaweza kukopeshwa hadi Shilingi Milioni 300 bila riba.
Akizungumza katika hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya Equity, Leah Ayoub, alisema mpango huo ulianza tangu mwaka 2021, ukiwalenga wajasiriamali na wasambazaji wa bidhaa za Azam wanaokabiliwa na changamoto za mitaji na riba.
“Tumekuja na suluhisho kwa wateja wetu kwa kushirikiana na Bakhresa Group ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara. Kupitia makubaliano haya, wafanyabiashara wa unga wanaweza kukopa fedha kwa ajili ya bidhaa mpaka Shilingi Milioni 300,” alisema Ayoub.
Kwa mujibu wa mpango huu, mkopo huo hautakuwa na riba. Badala yake, mteja atalipa kamisheni ya kati ya asilimia 0.5 hadi 1.5, na marejesho ya mkopo yanaweza kufanyika ndani ya kipindi cha siku saba hadi 30.
“Hii ni fursa ya kukuza mtaji kwa haraka. Tumetoa mwanya hata kwa wateja wasio na akaunti ya Equity kufungua moja kupitia simu zao za mkononi na kupata mkopo mara moja,” aliongeza Leah.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufiani, alisema huduma hii inaleta urahisi kwa wateja wao kwani inaweza kufanyika kidigitali kupitia mfumo wa SMS, bila kulazimika kwenda benki kufanya miamala.
“Huduma hii itasaidia sana wateja wetu hasa wadogo, hivyo nawasihi kuchangamkia fursa hii ya kipekee ya kuimarisha biashara zao,” alisema Sufiani.