Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 25 Septemba 2024, alitembelea kituo cha ununuzi wa mahindi kilichopo katika Soko Kuu, Mbinga mjini.
Akiwa katika kituo hicho, Rais Samia alipata maelezo kuhusu shughuli za usafishaji na upimaji wa mahindi zinazofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kabla ya kusalimiana na wananchi waliojitokeza kwa wingi kumlaki.
Katika hotuba yake, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kuwa wakulima wanapata faida kutokana na juhudi zao.
Aliwakumbusha wananchi kuwa hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, ambayo inalenga kuboresha maisha ya wakulima nchini.
Kwa mujibu wa maelekezo ya Rais, NFRA imeanzisha vituo vya ununuzi wa mahindi katika mikoa inayozalisha mazao haya kwa wingi, ikiwemo Ruvuma, Mbeya, na Njombe.
Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wakulima wanapata soko la uhakika kwa mazao yao bila kulazimika kusafirisha umbali mrefu, hali inayowapunguzia gharama na adha za usafirishaji.
Vilevile, mpango huo unalenga kuwalinda wakulima dhidi ya wafanyabiashara walanguzi wasio waaminifu ambao wamekuwa wakinunua mazao yao kwa bei ya chini isiyolingana na thamani halisi ya mazao hayo.
Aidha, Rais Samia alibainisha kuwa mpango wa NFRA ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali kuhakikisha kuwa mahindi yanayozalishwa nchini yanafikia soko la kimataifa, hatua ambayo itachangia kuongeza kipato kwa wakulima na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kwa kufanya hivyo, serikali imejipanga kuboresha usalama wa chakula na kukuza sekta ya kilimo nchini kwa kuzingatia mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.