Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, unatarajia kugawa bure zaidi ya miche laki moja ya miti ya asili inayoendana na mazingira ya eneo hilo. Hii ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha kuwa uoto wa asili unalindwa wilayani humo.
Kauli hiyo imetolewa na Bw. Charles Masawe, Mhifadhi wa Misitu Wilaya ya Tarime, wakati wa kikao cha wafanyabiashara wa mazao ya misitu kilichofanyika wilayani humo. Bw. Masawe alieleza kuwa zoezi la kugawa bure miche hiyo limekuwa likiendelezwa kwa wananchi wa maeneo husika kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi wa mazingira.
“Tupo hapa kwa ajili ya kikao cha kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa mazao ya misitu na tunaendelea kuwahamasisha juu ya umuhimu wa kutunza mazingira. Katika mkakati wetu, tumekuwa tukigawa miche ya miti na kwa mwaka wa fedha uliopita tuligawa miche elfu sabini na nne,” alisema Bw. Charles Masawe.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, alisisitiza umuhimu wa upandaji miti na utunzaji wake katika maeneo ya wananchi binafsi pamoja na maeneo yaliyotengwa. Pia, alihimiza kuachana na tabia ya uchomaji moto hovyo misituni na uvunaji holela wa miti.
“Niwaombe TFS na wasimamizi wote kuhakikisha wananchi wetu wanapata elimu sahihi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira. Badala ya kuwaonea wananchi, ni muhimu kuongeza nguvu katika kutoa elimu zaidi,” alisema Meja Edward Gowele.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo waliipongeza TFS kwa kutoa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira na waliiomba serikali kuendelea na juhudi za kutoa elimu itakayosaidia kuondoa migongano kati ya wananchi na wahifadhi.