Zaidi ya nchi 30 zimethibitisha kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Swahili International Tourism Expo (SITE) yanayotarajiwa kufanyika nchini Tanzania kuanzia Julai 11 hadi Oktoba 13, 2024.
Maonesho hayo, yenye kaulimbiu ya mwaka huu “Tembelea Tanzania kwa Uwekezaji Endelevu na Utalii Usioharibu Mazingira”, yatalenga kuhamasisha uwekezaji endelevu katika sekta ya utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Ephraim Mafuru, alieleza kuwa maandalizi ya maonesho hayo, yatakayofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, yako katika hatua za mwisho. Alifafanua kuwa maonesho haya ni fursa muhimu kwa Tanzania kufungua masoko mapya ya watalii kutoka nchi ambazo bado hazileti idadi kubwa ya watalii licha ya kuwa na idadi kubwa ya watu.
“Kuanzia Julai 11 hadi Oktoba 13, tutakuwa na maonesho makubwa, yanayojulikana kama Swahili International Tourism Expo (SITE 2024), ambayo yatafanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam. Lengo kuu ni kuimarisha mtandao wa kibiashara kwa wafanyabiashara wa sekta ya utalii,” alisema Mafuru.
Aliongeza kuwa sekta yoyote ya biashara ina mnyororo wa thamani; upande mmoja kuna watoa huduma na bidhaa, huku upande wa pili wakiwa ni wanunuzi. Hadi sasa, zaidi ya wadau 145 kutoka nchi 33 wameshathibitisha ushiriki wao, zikiwemo nchi zinazolengwa kimkakati.
Mafuru alizitaja baadhi ya nchi zilizothibitisha kushiriki maonesho hayo kuwa ni pamoja na China, Denmark, Finland, Japan, Afrika Kusini, Kenya, Ethiopia, India, Oman, Uholanzi, Nigeria, Brazil, Ujerumani, Uganda, na Lesotho.
Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni maonesho ya bidhaa na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya utalii, ambapo wanunuzi watapata nafasi ya kukutana na wazalishaji na watoa huduma ili kuimarisha mnyororo wa thamani. Pia, kutakuwepo na jukwaa la uwekezaji ambalo litatoa taarifa sahihi kwa wawekezaji wanaotaka kuingia katika sekta hiyo.
“Maonesho haya ni ya kipekee, kwani ni makubwa zaidi kwa Tanzania na hata kwa ukanda wa Afrika Mashariki,” alibainisha Mafuru.
Aliongeza kuwa TTB itashirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuhakikisha washiriki wanapata taarifa za kina kuhusu mazingira ya uwekezaji, kodi, na masuala ya kifedha yanayohusu sekta ya utalii.