Mbunge wa Jimbo la Msalala, Mheshimiwa Iddi Kassim Iddi, ameshiriki mahafali ya 20 ya Shule ya Msingi Kakola B, ambapo aligusia juhudi za Serikali za kuendelea kuboresha mazingira ya elimu, likiwemo suala la kuongeza vyumba vya madarasa na madawati.
Katika hotuba yake, Mbunge Iddi alieleza changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Kakola B, ambapo kwa sasa shule hiyo inahudumia wanafunzi 3,000. Akizungumza na wazazi waliokuwepo kwenye mahafali, aliwataka kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa kwa kuchagua viongozi makini watakaosaidia kutatua matatizo na changamoto za elimu na maendeleo ya jamii.
“Ni ukweli kwamba tumeweza kutatua changamoto ya madarasa kwa shule za sekondari, na sasa tunaelekeza nguvu kwenye shule za msingi ili kuhakikisha tunamaliza tatizo hili,” alisema Mbunge Iddi.
Mbunge Iddi pia alizungumzia suala la upungufu wa dawa, akibainisha kuwa tayari Serikali imetenga shilingi milioni mia nne (400M) kwa ajili ya kununua madawati. Alieleza kuwa tayari ameanza mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ili kushughulikia tatizo hilo. Kuhusu msongamano wa wanafunzi, alisisitiza kuwa shule ya sasa imejaa, hivyo kuna umuhimu wa kujenga shule mpya katika eneo jingine.
“Ni wakati sahihi kwa wazazi kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha tunaanza mchakato wa ujenzi wa shule nyingine haraka iwezekanavyo,” alihitimisha Mbunge Iddi.
Tukio hilo la mahafali lilihudhuriwa na viongozi wa eneo hilo pamoja na wazazi, ambao walionesha utayari wao wa kushirikiana na Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu.