Na Takdir Ali. Maelezo.
Waratibu wa jinsia kisiwani Pemba wametakiwa kuendelea kutoa elimu ya udhalilishaji katika Sheria zao ili Wananchi waweze kutambua athari, viashiria na njia bora za kujikinga na vitendo hivyo.
Wito huo uetolewa na Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Siti Abasi Ali wakati alipokuwa akizungumza na Waratibu wa masuala ya jinsia Mkoa wa Kusini Pemba huko Gombani Wilaya ya Chakechake.
Amesema elimu hiyo itasaidia Wananchi kuacha muhali na badala yake kuwafichuwa watakaowabaini kujihusisha na vitendo hivyo.
‘‘Wananchi waelewe kwamba saula la kuoneana muhali limepitwa na wakati, sisi tunachokuombeni ni kuunga mkono mikakati iliopangwa na Serikali ya awamu ya nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ,katika kutokomeza janga hili’’alisema Mkurugenzi Siti.
Aidha amesema Viongozi wa Nchi wamekuwa wadau wakubwa wa kupinga vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Hivyo amewataka Waratibu hao kutimiza wajibu wao kwa kuwaunga mkono Viongozi wao ili kuhakikisha mapambano hayo yanazidi yanaendelea.
Nae Afisa mendeleo ya jamii, jinsia na Watoto Wilaya ya Chakechake Salma Khamis Haji amesema kikao hicho kimewajengea ari, hamasa na motisha katika utendaji wa kazi jambo ambalo litapelekea kufanya kazi kwa ufanisi.
Hata hivyo amewashukuru Viongozi wa Idara ya maendeleo ya jamii, jinsia na Watoto kwa kuwaweka pamoja na kubadilishana mawazo kuhusiana na vitendo hivyo.
Jumla ya Waratibu 68 wa jinsia ndani Mkoa wa Kusini Pemba wameshiriki kikao hicho na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Ukatili na Udhalilishaji wa kijinsia katika Shehia zao.